WAKATI wanachama wa klabu ya Simba waliouondoa madarakani utawala wa
Ismail Aden Rage wakijipanga kuwasilisha ripoti yao Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), uongozi umekimbilia katika shirikisho hilo kuomba
suluhu.
Wanachama zaidi ya 700, walikutana juzi kwenye Hoteli ya Starlight
jijini Dar es Salaam na kuazimia kwa pamoja kuung’oa madarakani uongozi
wa Rage, ambapo walitarajia jana jioni au leo asubuhi kuwasilisha ripoti
yao TFF na Ofisi ya Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo.
Katika uamuzi huo, wanachama hao waliwateua Zacharia Hans Poppe na
Rahma Al Kharoos kuongoza klabu hiyo kwa muda hadi watakapopatikana
viongozi wengine. Hata hivyo, Poppe katangaza kutotambua uamuzi huo.
Akizungumza jana, mmoja wa waratibu wa mkutano huo,
Ustadh Masudi, alisema kwamba wako katika hatua za mwisho za kuiandaa
ripoti hiyo kabla ya kuiwasilisha kwenye mamlaka husika.
“Unajua suala hili ni la kisheria zaidi, hivyo tunahitaji kulifanya
kwa umakini mkubwa, kwa sasa tuko katika hatua za mwishomwisho kuandaa
hiyo ripoti, tukimaliza tutaiwasilisha hii leo na ikishindakana
tutaipeleka kesho,” alisema.
Kuhusiana na Poppe kugomea kuteuliwa kwake, Ustadh alisema kuwa
hawalitambui hilo, kwani amefanya hivyo kwa kuzungumza na vyombo vya
habari tu na si kuwakatalia wanachama.
“Hapo tunasubiri uamuzi wa kisheria, kama mkutano ulikuwa halali Hans
Poppe itabidi aitishe mkutano wa kukana kuteuliwa kwake na sisi
tutateuwa wengine,” alisema.
Akizungumzia suala hilo la wanachama jana, Ofisa Habari wa TFF,
Boniface Wambura, alisema watatoa tamko watakapoipata ripoti hiyo, huku
akibainisha kupokea barua ya uongozi ulioondolewa madarakani.
“Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea barua kutoka
uongozi wa Simba, ikielezea kutotambua mkutano ulioandaliwa na
wanaodaiwa kuwa wanachama wake na kufanyika jana (juzi), ukumbi wa
Starlight, Dar es Salaam,” alisema.
Wambura alisema vilevile katika barua hiyo, uongozi wa Simba umeahidi
kuitisha mkutano wa wanachama wake utakaoitishwa na mwenyekiti wake kwa
mujibu wa katiba ya klabu hiyo.
Alisema kutokana na hali hiyo, TFF imeitisha mara moja kikao cha
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji chini ya uenyekiti wa
Wakili Alex Mgongolwa, kwa ajili ya kutoa mwongozo kwa matukio ya aina
hiyo.
“Hata hivyo, TFF tunasisitiza kwa wanachama wetu ikiwemo Simba kuwa
wanachama wanapotaka kufanya uamuzi wowote ule, wanatakiwa kuzingatia
katiba na kanuni zilizopo,” alisema.
Katika mkutano wa juzi, mwenyekiti wa mkutano huo, Dk. Mohamedi
Wandwi, alisema kuwa Hans Pope na Rahma Al Kharoos watateua wajumbe wa
kuwasaidia na wataitisha mkutano mkuu wa uchaguzi baada ya Ligi Kuu
Tanzania Bara kumalizika.
“Ibara ya 16(g) ya Katiba ya klabu ya Simba, inatoa mamlaka ya mkutano
huu kuunda chombo kitakachosimamia kuanzia kesho mpaka uchaguzi
utakapofanyika, na tumewachagua Zakaria Hans Pope na Rahma Al Kharoos
kuongoza kamati ya muda ya Simba mpaka ligi itakapomalizika,” alisema
Dk. Wandwi.
Alisema kuwa katiba ya Simba inatoa siku 90 kuitishwa kwa mkutano mkuu
wa uchaguzi, lakini kwa kuwa ligi bado inaendelea, wameipa kamati ya
muda hadi ligi itakapomalizika kuitisha mkutano mkuu.
No comments:
Post a Comment