ASKARI polisi wa usalama barabarani, WP.2492 PC, Elikiza Nnko,
amekufa baada ya kugongwa na gari alipokuwa akiuelekeza msafara wa Rais
Jakaya Kikwete.
Ajali hiyo mbaya ilitokea jana jijini Dar es Salaam eneo la Bamaga
katika makutano ya barabara ya Bagamoyo na Shekilango ambapo askari huyo
aligongwa na gari lenye namba T. 328 BML aina ya Toyota Land Rover Mali
ya kanisa la Tanzania Asemblies of God.
Msafara wa Rais Kikwete uliokuwa ukielekea Mwenge ambapo kiongozi huyo alikuwa akikagua shughuli za maendeleo jijini humo.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kinondoni, Charles Kenyela, alisema ajali hiyo ilitokea saa 7:00 mchana
baada ya WP Elikiza kuongoza vema msafara wa Rais.
Alisema baada ya msafara huo kupita, lilitokea gari hilo lililokuwa
katika mwendo kasi na kuingilia msafara hali iliyosababisha ajali hiyo.
“Hatujampata dereva kwa kuwa hakusimama na tunawaomba wananchi
wasaidie ili tumpate, pia hali hii ya kuingilia misafara siyo nzuri,”
alisema.
Mbali na ajali hiyo, msafara huo wakati ukiondoka eneo la Kipawa
ulikumbana na mabango yaliyokuwa yakilalamikia hali ngumu ya maisha,
ubovu wa barabara na kuongezeka kwa uhalifu nchini.
Moja ya mabango hayo lilisomeka: “Tumechoka na umaskini, pamoja na ongezeko la uhalifu na ujambazi.”
Mapema katika ziara yake, Rais Kikwete akiwa Kipawa alifungua chuo cha
Veta kitakachotoa elimu ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Aliwataka wanasiasa kuacha tabia ya kuwadanganya wananchi kuwa mikopo ya maendeleo inayopatiwa Tanzania haiwasaidii.
Rais alisema badala yake wawaelimishe umuhimu wa kutumia vizuri miradi inayopatikana kutokana na mikopo hiyo.
Alisema kwa sasa wanasiasa wamekuwa wakiwatisha wananchi kwa kudai
kuwa kila mmoja anadaiwa sh 400,000 pasipo kuwaambia fedha hizo
zitalipwa kwa muda gani.
Alitolea mfano daraja la Mto Malagalasi na kusema riba itakayolipwa
kutokana na mkopo wa ujenzi wa daraja hilo ni asilimia 0.02, ambapo deni
lake litaanza kulipwa baada ya miaka 10 huku mkopo mzima ukichukua
miaka 40 kumalizika.
Kuhusu chuo hicho, Rais Kikwete alisema mahitaji ya Tehama
yanaongezeka kila siku kutokana na mabadiliko chanya yanayoendelea
duniani, serikali imeanzisha mamlaka ya habari yenye kuratibu na
kuendeleza matumizi ya Tehama.
No comments:
Post a Comment