Vatican City. Ulinzi mkali umeandaliwa kwa viongozi mbalimbali
wa kiserikali na wale wa kidini duniani waliowasili jijini Vatican, kwa
misa maalumu ya kutawazwa kwa Papa Francis leo.
Waumini na wageni milioni moja akiwamo Balozi wa Tanzania nchini Italia, Dk James Msekela, wanatarajiwa kuhudhuria misa hiyo itakayofanyika kwenye Viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.
Baada ya Papa Francis kutawazwa, ataanza rasmi kazi ngumu ya kuliongoza Kanisa Katoliki lenye waumini wengi na ambalo limekumbwa na mizozo kadhaa ikiwamo ya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya makasisi.
Kiongozi huyo alichaguliwa Jumatano iliyopita kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Papa Benedict XVI, aliyejiuzulu Februari 28, mwaka huu.
Misa ya kutawazwa kwa Papa Francis, imeifanya Mamlaka ya Jiji la Rome kuandaa ulinzi mkali kwa watu wote ambao wanatarajiwa kuhudhuria tukio hilo la kihistoria.
Tayari, Papa Francis ameduwaza wengi kwa kauli na vitendo vyake vingi ambavyo vinamwonyesha kama kiongozi asiyependa makuu na ambaye pia anatarajiwa kubadili uendeshaji wa kanisa hilo lenye waumini 1.2 bilioni.
Miongoni mwa wageni maalumu waliowasili Italia ni Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Mkatoliki ambaye hii ni mara yake ya pili kukiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya (EU) dhidi ya utawala wake.
Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden ambaye pia ni muumini wa kanisa hilo anatarajiwa kuhudhuria. Misa hiyo imewekwa rasmi kwa kumbukumbu ya Mtakatifu Yosefu, ambaye ndiye msimamizi wa kiimani wa Taifa la Italia, mahali iliko Vatican.
Wengine ni Rais wa Argentina, Cristina Kirchner na mpinzani wa Papa Francis ambaye jana alitarajiwa kukutana naye kwa mazungumzo ya faragha. Wawili hao wamekuwa wakisigana katika masuala mengine yakiwamo ndoa za mashoga na utoaji mimba.
Rais wa Brazil, Dilma Rousseff amewasili pia kama ilivyo kwa mwenzake wa Mexico, Enrique Pena Nieto. Pia, Rais wa Chile, Sebastian Pinera aliwasili Rome tangu Jumapili kwa misa ya kwanza ya Papa Francis. Rais huyo ni miongoni mwa wageni maarufu. Yumo pia Makamu wa Rais wa Ufilipino, Jejomar Binay akimwakilisha Rais Benigno Aquino III.
Orodha hiyo inawajumuisha pia Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Waziri Mkuu wa Hispania, Mariano Rajoy , Waziri Mkuu wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault , Rais wa EU, Herman Van Rompuy, Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya, Jose Manuel Barroso.
Wengine ni mwakilishi wa Kanisa la Anglikana, Askofu Mkuu wa York, John Sentamu. Pia, Ibrahim Isaac Sidrak, kutoka Jumuiya ya Wakoptiki ya Kanisa Katoliki, Alexandria, Misri na Metropolitan Hilarion, ambaye ni mkuu msaidizi wa Kanisa la Orthodox , Russia.
*Ndyesumbilai Florian kwa msaada wa mtandao
No comments:
Post a Comment