Naibu Katibu Mkuu CHADEMA Tanzania Bara na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Mh. Zitto Kabwe.
KATIKA gazeti la Mtanzania toleo na. 7269 la Jumatano Machi 27, 2013
kuna habari yenye kichwa chenye maneno ‘SIRI YA KUUWAWA ZITTO YAFICHUKA’
na vichwa vidogo ‘yadaiwa ilipangwa anyweshwe sumu hotelini’ Dk. Slaa
atajwa kumtuma Saanane kummaliza’. Habari hii imeniletea usumbufu mkubwa
kwani ndugu, jamaa, marafiki na wapiga kura wangu, wamejazwa na
wasiwasi mkubwa sana kwamba ninaweza kuuwawa.
Napenda kusema yafuatayo:
Moja, sijawahi katika maisha yangu yote
kukutana na mtu anayeitwa Ben Saanane na hivyo hicho kikao ambacho
inasemekana nilikuwa naye na akajaribu kunipa sumu hakijawahi kutokea.
Imetajwa Hoteli ya Lunch Time ambayo sio tu sijawahi kufika, pia hata
siijui ipo wapi. Haijawahi kutokea mimi kufanya kikao cha pamoja na Ben
Saanane, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni
ya kufikirika na hivyo naomba mwandishi ahakikishe kuwa vyanzo vyake
vya habari vimempa habari sahihi.
Pili, Siamini kamwe kuwa Katibu Mkuu wa chama changu anaweza kupanga
kuniua maana hana sababu ya kufanya hivyo. Napenda kurudia kusema kwamba
mimi ninaamini kuwa kila nafsi itaonja mauti. Kila mtu atakufa. Kama
nitakufa kwa kuuwawa na mtu mwingine ndio itakuwa nimeandikiwa hivyo na
Mungu. Ndio maana hata siku moja silalamiki kuhusu vitisho vya kuuwawa
nk. Kama kuna mtu anafikiria kuwa kumuua Zitto ndio furaha ya maisha
yake atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza kufa kimwili lakini
mawazo, fikra na maono ya Zitto yataishi tu. Siogopi kufa maana maisha
niliyoyachagua ndio haya ambayo yamejaa vitisho. Muhimu kwangu ni
kufanya kazi zangu kwa bidii, uhodari na uaminifu. Siku zote nitasimamia
ukweli bila kujali uchungu wa ukweli huo.
Tatu, nawashauri watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine
watumie muda wao kujenga vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia
masuala ya chama ambacho wao sio wanachama tena. Kama mtu kaamua kuhama
CHADEMA anapoteza haki ya kujadili masuala ya CHADEMA maana kama
angekuwa anapenda kuyajadili asingehama. Naonya mtu yeyote ambaye
anatumia jina langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa. CHADEMA sio
pango la watesaji wala wauaji. Kama kuna mwanachama wa chama kingine
cha siasa anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu
aende kwenye vyombo vya sheria kumshtaki. Matendo ya mtu mmoja
yasifanyiwe propaganda kama ni malengo ya taasisi.
Nne, Nawashauri viongozi wenzangu wa CHADEMA na hasa wanachama
tutumie muda wetu kujenga mshikamano ndani ya chama. Fitna, majungu,
uongo, uzandiki nk kamwe havijengi chama. Chama chetu lazima kiwe mfano
bora wa kuheshimu demokrasia na haki za binaadamu. Wananchi hawawezi
kutoa dola kwa chama chenye mifarakano. Tusiruhusu kugawanywa kwa
matakwa ya watu wachache. Tusimamie misingi ya kuanzishwa chama chetu.
Imetolewa na Naibu Katibu Mkuu CHADEMA Tanzania Bara,
Mh. Zitto Z Kabwe
No comments:
Post a Comment