WAANDISHI wa habari wawili na Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya
Handeni, mkoani Tanga wamefariki dunia jana na watu wengine watatu
kujeruhiwa wakiwa kwenye msafara wa
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo
Rweyemamu, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na
kupinduka.
Waandishi wa habari waliofariki dunia katika ajali hiyo ni Hussein
Semdoe anayeandikia magazeti ya Nipashe na Mwananchi, Bwanga Hamis
Bwanga anayeandikia gazeti la Uhuru na Radio Abood, huku Ofisa Uhamiaji
akitajwa kwa jina la Mariamu Hassan.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo, aliyekuwa katika msafara huo
alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana na kuwataja majeruhi kuwa ni
Mlawa Mataka, aliyekuwa akiendesha gari lililopata ajali STK 4673 Toyota
Land Cruiser V8, Mshauri wa Mgambo wa Wilaya ya
Handeni, Sajenti
Athanas Paul pamoja na Ofisa Misitu wa wilaya hiyo, Mlowe Natorin.
Muhingo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea eneo la Ndolwa wilayani hapa kulikokuwa na kilele cha shughuli ya upandaji miti.
Alisema gari lililopata ajali ni la Mkurugenzi wa Wilaya ya Handeni na
lilipofika katika eneo la Misima lilipata pancha na kuacha njia, hali
iliyosababisha watu waliokuwa kwenye gari kurushwa nje na kusababisha
mauti kwa baadhi yao.
Aliongeza kuwa katika msafara huo uliokuwa unatoka mjini Handeni,
mkurugenzi wa wilaya hiyo hakuwemo katika gari lililopata ajali.
Muhingo alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Handeni na majeruhi wakipatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
No comments:
Post a Comment