Habari na Tanzania Daima.
MGOGORO ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
(UVCCM), unazidi kupamba moto huku mikakati ya kumng’oa Mwenyekiti,
Sadifa Juma Khamis na
Makamu wake, Mboni Mhita, ikizidi kuanikwa.
Mikakati hiyo inadaiwa kusukwa na kundi moja ndani ya CCM, ikihusishwa na mbio za urais za mwaka 2015.
Uchunguzi wa Tanzania Daima, umebaini kuwapo kwa kundi ambalo
Mwenyekiti wa UVCCM, analituhumu kupanga mikakati mbalimbali ya kumng’oa
katika nafasi hiyo kwa masilahi binafsi.
Mwanzoni mwa wiki hii, gazeti hili liliripoti kuhusu kundi hilo
linalotumia sababu za kuwepo vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa umoja
huo uliopita pamoja na madai kwamba mwenyekiti alighushi umri.
Kundi hilo linadaiwa kufadhiliwa na mmoja wa vigogo wa chama hicho
wanaotajwa kuusaka urais mwaka 2015 kwa udi na uvumba, ambaye pia ni
mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) mwenye uhusiano wa karibu na
Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete.
Chanzo chetu ndani ya UVCCM kimedokeza kuwa mjumbe huyo ndiye
analiwezesha kundi hilo kifedha katika mkakati huo wa kutaka kumng’oa
Sadifa kwa vile si miongoni mwa wafuasi wake katika kuelekea mbio za
urais za mwaka 2015.
Akizungumza na gazeti hili, Sadifa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Donge, alisema: “Kuna kundi la vijana wapatao kumi kutoka mikoa
mbalimbali (majina tunayo), wananifanyia fitina na kuniingilia katika
utendaji wangu wa kazi za kila siku kinyume cha katiba ya jumuiya yetu.
“Ninahisi kuwa kundi hili linasaidiwa na mtu mwenye nguvu au mwenye
mamlaka kwenye chama. Nasema hivyo kwa sababu sasa hii ni mara ya tatu,”
alisema.
Sadifa alisema kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi wao uliofanyika
mjini Dodoma, watu hao walikuja na mabango kwenye mapokezi yake jijini
Dar es Salaam ofisi ndogo za chama Lumumba.
Alisema kuwa kundi hilo liliandaa watu wakafanya fujo hadi kupigana, na kufikia hatua ya kutosalimiana sasa.
“Nimefika makao makuu juzi, nikakuta vijana watatu waliokuwepo hapo
nikawasalimia, lakini mwingine alitaka kunishambulia nikakimbilia
ofisini kwa Nape Nnauye,” alisema.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti kwa masharti ya
kutotajwa majina yao, baadhi ya wajumbe wa baraza hilo walisema: “UVCCM
kuna tatizo tena kubwa.” Kwamba kilichotokea na kinachotokea sasa ni
mwenyekiti wao kushindwa kujibu hoja.
“Tulihoji utaratibu aliotumia katika uteuzi wa makatibu kwenye jumuiya
yetu, akasema sisi tunataka kuchanganya mapenzi na kazi, kitu
kilichozua malumbano katika kikao chetu,” walisema.
Walidai kuwa kauli hiyo iliwaudhi na sasa hata kama hawana mpango wa
kumwondoa madarakani, atajiondoa mwenyewe kwa kushindwa kusimamia yale
ambayo aliahidi.
“Mwenyekiti wetu ni tatizo,” alisema mmoja wa wajumbe wa UVCCM huku
akionesha ujumbe mfupi wa simu ambao amewahi kutumiwa na mwenyekiti
huyo.
Ujumbe huo ulisomeka: “Usinitumie sms za kipumbavu, wananena respect
yourself, if you can not respect yourself no body will respect you…
ukianza nitamaliza.”
Mjumbe huyo aliongeza kuwa, Sadifa alishinda kwa rushwa, kwamba kila
mjumbe alipewa kati ya sh 50,000 hadi 100,000 ili kufanikisha uchaguzi.
“Mwenyekiti wa chama alikuja akaonya kuhusu rushwa, lakini alipotoka
tu, miguu yake ikafutwa kwa kugawiwa sh 20,000 za haraka haraka kwa kila
mjumbe,” alisema.
Alipotafutwa mmoja wa wajumbe wa kundi linalotuhumiwa na mwenyekiti,
alisema: “UVCCM ni mbovu yote, si suala la taasisi, huu ndio msimamo
wangu”.
No comments:
Post a Comment