SAKATA la Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick
Rwezaula kushtakiwa kwa makosa ya ugaidi, limeibua mvutano mkali bungeni
huku wabunge wakishambuliana kwa maneno makali.
Mvutano huo uliibuka jana wakati wa kujadili hotuba ya bajeti ya
Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/2014 ambapo Mbunge wa
Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) alichafua hewa wakati
akichangia na kudai kuwa aliyerekodi video ya Lwakatare yupo tayari kuja
kutoa ushahidi.
Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) aliliambia
Bunge kuwa CHADEMA wasihangaike kujitetea kwa swala la Lwakatare kwani
ushahidi wote kuhusu video hiyo upo na kwamba yuko tayari kuutoa
bungeni, duniani na mbinguni.
“Nataka nitoe ufafanuzi kuhusu suala la ugaidi ambalo Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe amezungumza kwenye hotuba yake hapa bungeni
jana. Aliyerekodi mkanda yupo na mimi niko tayari kuhojiwa popote hata
mbinguni,” alisema Mwigulu na kuibua nderemo kutoka kwa wabunge wa CCM.
Mwigulu alionyesha karatasi aliyodai kuwa ilitumiwa na Lwakatare
kupanga kile alichodai kuwa ni mkakati wa mauaji akisema huo ndiyo
mkakati wa CHADEMA kupanga mauaji na kwamba viongozi wakuu wa chama
hicho wanapaswa kushtakiwa.
Bila kujali kwamba suala hilo liko mahakamani wala ni kinyume cha
kanuni za Bunge kumtaja mbunge mwingine kwa jina akimtuhumu, Mwigulu
alisema anaishangaa CHADEMA kumtaka yeye aunganishwe kwenye kesi kwa
kuwa na mawasiliano na mmoja wa watuhumiwa wakati hata wao wana
mawasiliano na Lwakatare.
“Alisema Mbowe hapa jana kuwa mimi napaswa kushtakiwa kwa ugaidi,
ingawa simuoni hapa ndani labda tayari amekwishakamatwa na polisi,
lakini nataka kusema kuwa watu hawa ni waongo na wanafiki. Wanapanga
mauaji halafu wanakuja hapa kuwahadaa wananchi kuwa wanapinga ugaidi,”
alidai.
Hatua hiyo ya Mwigulu kumtaja Mbowe kwa jina na chama chake kuwa ni
magaidi, iliwashtua baadhi ya wabunge wakishangaa kuona Spika wa Bunge,
Anne Makinda akishindwa kutumia kanuni kumbana na kumtaka afute kauli
ana atoe uthibitisho.
Baada ya kuona Makinda anakuwa na kigugumizi, baadhi ya wabunge wa
CHADEMA, Joseph Selasini (Rombo), Mustafa Akunaay (Mbulu), Pauline
Gekul (Viti Maalumu) walijaribu kusimama kuomba mwongozo lakini
walikataliwa.
Hata hivyo, Akunaay aliendelea kuomba mwongozo akitaka Mwigulu aache
kuzungumzia suala hilo kwa vile liko mahakamani, lakini Spika Makinda
alisimama na kusema kwamba kama ni suala la kanuni zifuatwe kwa wote.
Spika Makinda ambaye alionekana kukitetea chama chake cha CCM
alitumia mafumbo kuwajibu wabunge wa CHADEMA akiwataka kuacha tabia ya
mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu.
“Jana Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe alizungumzia suala
la ugaidi na kesi iliyopo mahakamani, hakuzuiliwa. Leo mnamzuia
Mwigulu. Kama ni kanuni ziwe kwa wote si mkuki kwa nguruwe halafu kwa
wengine...,” alisema.
Baada ya Mwigulu kuchangia ndipo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu (CHADEMA) alipata nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu na
kuzungumzia maeneo matatu ya elimu, usalama wa nchi na katiba mpya.
Katika suala la usalama, Lissu alijielekeza moja kwa moja kupangua
makombora ya Mwigulu bila kumtaja kwa jina, akisema Jeshi la Polisi
limekuwa na mawasiliano na baadhi ya watu ndani ya Bunge kufanya vitendo
vya kigaidi na kuwapakazia watu wengine.
“Kwa muda mrefu Jeshi la Polisi limekuwa likituhumiwa kufanya vitendo
vya uhalifu na kushirikiana na watu humu ndani kupanga vitendo vya
kigaidi na kuwasingizia watu wasio na hatia. Hii haikubaliki,” alisema
Lissu.
Lissu alisema kuwa mmoja wa watuhumiwa wa ugaidi wanaoendelea
kushikiliwa mahabusu amekuwa akifanya mawasiliano ya simu na mmoja kati
ya wabunge kupanga njama za ugaidi na kuwabambikia watu wasio na
hatia.
Alienda mbali kwa kusema kuwa kiongozi huyo ambaye yumo ndani ya
Bunge, alituma pesa kwa njia ya simu kwa mmoja wa watuhumiwa hao
wa ugaidi kwa ajili ya kupanga ugaidi.
Wakati akiendelea na hotuba yake, Mbunge wa Viti Maalumu, Anna
Abdallah (CCM) aliomba mwongozo wa Spika kuhoji kama Lissu ana ushahidi
wa mambo anayosema.
Alipotakiwa na Spika kujibu swali hilo, Lissu alisema mawasiliano ya
kwanza kati ya kiongozi huyo na mtuhumiwa mmoja wa ugaidi, yalifanyika
Januari 24 mwaka jana.
“Mawasiliano ya pili yalifanyika Desemba mwaka jana ambapo kiongozi
huyo alituma pesa kwa mtuhumiwa huyo. Mheshimiwa Spika tuna ushahidi wa
kutosha kuhusu hilo,” alisema Lissu.
Hata hivyo, hatua ya Spika kukatiza hotuba ya Lissu na kumpatia
nafasi Abdallah kuomba mwongozo ililalamikiwa na wabunge wa upinzani
ambapo wengine walikuwa wakizomea na kudai kuwa anapendelea.
Lissu aliendelea na mchango wake akisema “sheria ya ugaidi inasema
anayetoa fedha kufadhili ugaidi naye ni gaidi, akamatwe, afungwe.”
Mbali ya kuzungumzia suala hilo la ugaidi, Lissu alisisitiza kauli ya
Mbowe juzi kuwa CHADEMA haitashiriki kwenye mchakato wa katiba kama
kasoro zilizoainishwa hazitarekebishwa.
Alisema CHADEMA ikijitoa haitabaki kimya, bali itazunguka nchi nzima kuwataka wananchi kutoipigia kura ya ndiyo.
Lissu alisema Kenya na Zimbabwe zilishamwaga damu kutokana na katiba
na kuitahadharisha serikali kuwa makini na mchakato huo.
Pia alijadili suala la elimu akisema kuwa sasa ni wakati wa kuwajibishana na sio kutafuta mchawi.
“Waziri Mkuu amesema kwenye hotuba yake juzi kwamba tusitafute mchawi
wala sio wakati wa kulaumiana. Mimi nakubali kwamba huo si wakati wa
kulaumiana bali wa kuwajibishana,” alisema Lissu.
Alionesha ripoti ya serikali ya mwaka 2010 iliyochunguza chanzo cha
kufeli kwa matokeo ya kidato cha nne, lakini haijafanyiwa kazi wala
haijatangazwa hadharani.
“Ripoti hii Waziri Mkuu anaijua, hajaifanyia kazi, leo ameunda tume
nyingine. CHADEMA tunasema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi
afukuzwe, Waziri Mkuu afukuzwe, wameshindwa kazi,” alisema.
Alisema kama rais hataki kumwajibisha, Bunge lipige kura ya kutokuwa na imani naye.
Baada ya Lissu kumaliza kujadili hoja hiyo, Spika Makinda aliitaka
Kamati ya Kanuni kukutana kwa dharura kujadili ukiukwaji huo wa kanuni
mpya walizojiwekea, na hivyo kufikia hatua ya wabunge kujadili jambo
lililoko mahakamani.
No comments:
Post a Comment