Akizungumza kwa simu jana, Kagasheki ambaye pia ni Mbunge wa
Bukoba Mjini (CCM), alisema Serikali imeamua kuchukua kilomita za mraba
1,500 kati ya kilomita za mraba 4,000 za eneo la Loliondo.
Waziri Kagasheki
Alisema ilifikia uamuzi huo ili kulifanya eneo hilo kuwa pori tengefu kwa ajili ya kusaidia wanyama kuzaliana na kupata malisho, hatua ambayo inapingwa na wakazi wa eneo hilo.
Waziri huyo alisema kuwa Nchemba, ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, anapaswa kuelewa kuwa Serikali haikukurupuka kuchukua uamuzi.
Alisema matamshi ya kiongozi huyo wa CCM hayawezi kuwa msimamo wa chama kwani viongozi hao walitumwa kwenda Loliondo kukusanya maoni na kisha kuyawasilisha kwenye vikao vyake halali na siyo kutumia mikutano ya hadhara kutoa uamuzi.
“Hayo maneno kama kweli yamesemwa na Nchemba, basi hayo ni mawazo yake na wala siyo msimamo wa chama. Mimi najua chama chetu kina taratibu za kujadili mambo na siyo kuanza kuzungumza nje ya vikao,” alisema na kuongeza:
“Ninachoweza kusisitiza hapa ni kwamba huyu (Nchemba) hakutumwa na chama kutoa maagizo, yeye alipaswa kuwasilisha maelezo yake kwenye vikao… Kwa maana hiyo uamuzi wa Serikali bado uko palepale na haya yanayosemwa ni ya kwao.”
Hata hivyo, uamuzi wa Serikali unapingwa vikali na wakazi wa Loliondo kwa madai kuwa maeneo inayoyachukua yana vijiji vyenye hatimiliki.
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliunda kamati kufuatilia suala hilo iliyowahusisha Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Mbunge wa Longido, Lekule Laizer na Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.
Mbunge Telele na kujiuzulu
Mbunge wa Ngorongoro (CCM), Saning’o Ole Telele amesisitiza kuwa uamuzi wake wa kujiuzulu pamoja na madiwani wake, upo palepale ikiwa Serikali itaendelea kung’ang’ania kuchukua ardhi hiyo bila ridhaa ya wananchi.
Akizungumza jana, Telele alisema kwa sasa wameamua kupeleka mgogoro huo katika chama tawala ili kichukue hatua akiamini kuwa haki ya wananchi wa Loliondo wanaopinga ardhi yao kuchukuliwa itapatikana.
Wananchi wa Tarafa ya Loliondo na Sale, wanapinga hatua ya Serikali kuchukua ardhi hiyo iliyopo katika vijiji vinane kwa madai kuwa ndiyo tegemeo lao la upatikanaji wa huduma muhimu za maji na ufugaji na kwamba iwapo litachukuliwa, maisha ya watu zaidi ya 65,000, ambao ni wafugaji yatakuwa shakani.
No comments:
Post a Comment