Jeshi la Polisi Mkoani hapa limemkamata mtu mmoja aitwaye Ally
Rashid Salimu (23) Mwendesha pikipiki za abiria maarufu kwa jina la
“Boda Boda” mkazi wa kata ya Sombetini jijini hapa akiwa na bunduki aina
ya shortgun Mossberg yenye namba T292166 ikiwa na risasi
sita.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana saa 5:30
asubuhi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi
(ACP) Liberatus Sabas alisema kwamba, tukio hilo lilitokea juzi tarehe
28.04.2013 muda wa saa 3:00 asubuhi katika maeneo ya Shamsi yaliyopo
jijini hapa.
Alisema siku ya tukio dereva huyo wa pikipiki akiwa katika eneo
hilo alikuwa anaendesha pikipiki aina ya Skymark yenye namba za usajili
T. 615 BZL huku akiwa amebeba begi lilionekana kutuna sana, ndipo askari
waliokuwa doria katika eneo hilo walimtilia shaka na kisha kumfuatilia
na kufanikiwa kumsimamisha.
“Mara baada ya kumsimamisha askari hao
walipekua begi hilo na kukuta silaha hiyo ikiwa na risasi sita na kisha
kumfikisha mtuhumiwa huyo katika kituo kikuu cha polisi cha hapa Arusha
mjini”. Alifafanua Kamanda Sabas.
Kamanda Sabas alisema upelelezi juu ya tukio hilo bado unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani pindi utakapokamilika.
Tukio hilo la ukamataji wa bunduki hiyo limekuja wiki tatu tu baada
ya jeshi hilo kukamata bastola moja pamoja na risasi 41 kutoka kwa
watuhumiwa waliokuwa wanahusishwa na matukio ya kumjeruhi Sister Mary
Shobana na kisha kumnyang’anya fedha taslimu Tsh 30,000,000/= (Milioni
thelathini) eneo la Notre Dame Njiro lililopo jijini hapa, fedha ambazo
alitoka kuchukua benki ya Exim tawi la Shoprite.
No comments:
Post a Comment