MREMBO wa Tanzania mwaka 1999, Hoyce Temu, leo anatarajiwa
kukutana na washiriki wanaowania taji la kitongoji cha Kigamboni,
‘Redd’s Miss Kigamboni 2013’ ili kuwapa nasaha mbalimbali kuhusiana na
sanaa hiyo.
Shindano la Redd’s Miss Kigamboni, linatarajiwa kufanyika kwenye
Ukumbi wa Navy Beach kuanzia saa 2:00 usiku hapa jijini Dar es Salaam,
Juni 7.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mratibu wa shindano hilo, Somoe
Ng’itu, alisema kuwa maandalizi yako katika hatua za mwisho na lengo la
kumualika Hoyce ni kuwapa nafasi warembo kujifunza mambo mbalimbali
yanayohusu sanaa hiyo.
Mratibu huyo alisema kuwa washiriki hao watajifunza mambo ya msingi
kupitia mrembo huyo ambaye pia atawapa uelewa wa mbinu watakazokutana
nazo kwenye mashindano ya kanda, taifa na baadaye fainali za dunia.
“Ni fursa ambayo tunatarajia warembo wetu wapate, nia ya kufanya hivi
ni kuwaandaa kufanya vizuri, tumejipanga kupata mafanikio zaidi ya
tuliyovuna mwaka jana,” alisema Somoe.
Aliongeza kuwa hadi sasa warembo 12 wanaendelea na mazoezi chini ya mkufunzi Blessing Ngowi.
Aliwataja washiriki hao kuwa ni pamoja na Rogathe Michael, Irene
Rajab, Magdalena Olotu, Latifa Mohammed, Axsaritha Vedastus, Angella
Lutataza, Sara Makembo, Amina Mussa, Ellen Sulle, Julieth Mwanri na
Rachel Reuben.
Alitoa wito kwa kampuni na taasisi mbalimbali, kudhamini shindano hilo
ambalo mwaka jana lilitoa mshindi katika kinyang’anyiro cha kanda ya
Temeke, ambaye ni Edda Sylivester.
Warembo watano watakaoshika nafasi za juu kwenye shindano hilo,
watapata nafasi ya kushiriki kinyang’anyiro cha Redd’s Miss Temeke
baadaye mwaka huu.
Wadhamini ambao wamethibitisha kusaidia shindano hilo ni pamoja na
Kampuni ya Bia Tanzania kupitia kinywaji cha Redd’s Premium Original,
Montage Limited, Clouds Media Group, Papa Z na Break Point.
Taji la Redd’s Miss Tanzania linashikiliwa na Brigitte Alfred wakati
Edda alifanikiwa kushika nafasi ya tatu kwenye fainali hizo za taifa
mwaka jana.
No comments:
Post a Comment