UGUNDUZI wa gesi asilia mkoani Mtwara umegeuka laana kwa wakazi wake wanaoishi maisha ya wasiwasi hivi sasa.
Sauti za milio ya mabomu, risasi, na vipigo ndivyo vinavyonekana
kushamiri zaidi kwenye mji huo uliosifika kwa amani na utulivu kwa muda
mrefu.
Idadi kubwa ya askari polisi na wanajeshi
wakiwa kwenye pikipiki na magari wakizunguka maeneo mbalimbali kwa
lengo la kudhibiti vurugu.
Wakati hali ikizidi kuwa tete mkoani humo, jana polisi wanadaiwa
kumuua kwa kumpiga risasi mjamzito aliyekuwa nyumbani kwake eneo la
Magomeni.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi
amethibitisha kupokea mwili wa mjamzito huyo ukiwa na tundu tumboni, na
hivyo kufanya idadi ya maiti zilizopokelewa hospitalini hapo kufikia
mbili na majeruhi 18.
“Ni kweli kwa leo tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa miezi saba, amepigwa risasi tumboni.
“Pia tumepokea mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Chuno, amevunjwa miguu yote kwa risasi,” alisema Dk. Ligula.
Habari ambazo Tanzania Daima ilizipata kutoka Mtwara jana, zilidai
polisi walishiriki kuchoma moto nyumba tatu za wananchi katika eneo hilo
na vibanda vya maduka kadhaa na kupora vitu vilivyomo ndani.
Chanzo kimoja kimedokeza kuwa maeneo ya Magomeni, Chikongola,
Nkanaledi na Mikindani, askari walikuwa wakiingia kwenye nyumba za watu
na kumkamata mtu yeyote hususan wanaume.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa uhalifu uliofanywa na askari hao uliamsha
hasira za wananchi jambo lililosababisha kutokea mapambano kati yao.
Baadhi ya vitu vinavyodaiwa kuibwa na askari hao kutoka kwenye maduka ni mchele, sukari, unga wa ngano na nguo.
Wakati polisi wakidaiwa kushiriki kwenye vitendo hivyo, huduma za
kijamii zimesimama hali inayochangia mambo kuzidi kuwa tete ndani ya
mkoa huo.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wakazi wa
Mtwara wamelalamikia kitendo cha askari wa Jeshi la Polisi kuingia
katika makazi yao, kuwapiga na kuwapora mali zao.
“Magomeni A hatuna amani, askari wanaingia majumbani mwetu, wanatupiga
na kutunyang’anya simu, yaani huku Magomeni hatuna amani kabisa,
tumepoteza watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi,” alisema Paulina
Idd.
“Majumba yetu yamechomwa moto wanaofanya fujo ni polisi wenyewe halafu
wanakuja wanatubaka na kuiba mali zetu, tunateseka sisi, yaani
tumechoka kabisa na serikali yenyewe,” aliongeza kusema.
Wakati wananchi wakilalamikia hali kutokuwa shwari, Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alisema hali ni nzuri na kuwataka
wakazi wake waendelee na shughuli zao kama kawaida.
Alipoulizwa kuhusu polisi kumuua mjamzito, kuchoma moto nyumba na
kuiba vitu, kamanda huyo alikataa kuyazungumzia hayo kwa madai
atapingana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Kamanda Sinzumwa alisema jana walimtarajia Waziri Nchimbi mkoani humo ili kuangalia hali ya mambo.
Wakazi wakimbia maeneo yao
Wakazi wa maeneo mbalimbali mjini Mtwara wamekimbia makazi yao
hususani wanawake na watoto na kuhamia hospitali ya rufaa kwa kuhofia
usalama wao huku wengi wao wakipotezana na ndugu zao.
Hali hiyo imetokea kufuatia kuwepo kwa milipuko ya mabomu katika
maeneo mbalimbali mjini humo huku huduma za kijamii zikiwa bado
zimesitishwa.
No comments:
Post a Comment