WABUNGE wameichachamalia mifuko ya hifadhi za jamii wakidai
inakusanya fedha nyingi kwa wanachama, lakini huduma zake hazikidhi
mahitaji na matarajio ya wahusika.
Hali hiyo ilijitokeza jana wakati wa semina kwa wabunge iliyoandaliwa
na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii
(SSRA) ikiwa ni ya pili kwa ajili ya kuwapa uelewa wabunge kuhusu
huduma za mifuko hiyo.
Katika michango yao, baadhi ya wabunge walielekeza malalamiko yao
mengi kwa Mfuko wa
Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wakisema kuwa
unawalenga zaidi matajiri.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keisy (CCM), ndiye alikuwa wa kwanza
kuishambulia NSSF akisema kuwa inakopesha matajiri ambao hata wakati
mwingine wanashindwa kulipa madeni hayo.
“Hii mifuko mikubwa ya NSSF, PPF na wengine wanajenga vijumba vya
hovyo vyenye vyumba viwili halafu wanawauzia wanachama kwa sh milioni
70. Huu ni wizi, hakuna nyumba ya vyumba viwili inaweza kuuzwa kwa
kiasi hicho,” alisema.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM) aliipa changamoto
mifuko hiyo kufikiria zaidi kwenye uwekezaji wa miradi ya kukuza uchumi
kama vile reli na umeme.
“Uwekezaji wa mifuko hii kila wakati ni kwenye majengo ambayo
kitaalamu hayakuzi uchumi, kwanini wasifikirie kujielekeza kwenye reli
na umeme,” alihoji.
Mbunge wa Viti Maalumu, Christowaja Mtinda (CHADEMA), alidai kuwa NSSF inawaibia wanachama kupitia nyumba inazowauzia.
“Mimi nimeuziwa nyumba kule Kijichi jijini Dar es Salaam kwa sh
milioni 103 halafu kila mwaka nakatwa sh 1.2 ambayo itakatwa baada ya
miaka 20, hiyo ni nyumba ya aina gani inaweza kulipiwa fedha kiasi
kikubwa hivyo?” alihoji.
Pia alihoji kuponi kwa ajili ya wanachama wa NSSF ambao wanatakiwa
kupata huduma za matibabu mbali na hospitali wazozichagua ili
kuwaondolea usumbufu.
Susan Kiwanga wa Viti Maalumu (CHADEMA) naye alihoji ni kwanini NSSF
iwalazimishe wanachama wake kukopa kupitia Saccos ilhali wakati wa
kujiunga hawapewi utaratibu huo.
Alizungumzia masharti ya fao la kujitoa yanayomtaka mwanachama awe
amefikisha miaka 60 akisema ni kuwatesa wategemezi kwani umri wa kuishi
Mtanzania ni miaka 47 na kwamba kwa masharti hayo mwanachama atakuwa
amekufa.
Mfuko mwingine ambao ulilalamikiwa na wabunge ni ule wa Bima ya Taifa
ya Afya (NHIF), wakisema kuwa dawa hazipatikani katika hospitali na
kwamba pia zinauzwa kwa bei kubwa ambayo ni mara mbili zaidi ya ile
halali.
Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile (CCM), Ally Keisy (CCM) na
Said Arfi wa Mpanda Mjini (CHADEMA), walitaka ufanyike utaratibu wa
kuwawezesha wananchi wote kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya.
Mifuko hiyo ambayo inasimamiwa na SSRA ni NSSF, PPF, PSPF, LAPF, GEPF
na NHIF ambayo jana wakuu wake walipata nafasi ya kueleza huduma zao
kwa wabunge.
Akijibu hoja za wabunge, Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka alisema
kuwa bado mchakato wa kuhusu fao la kujitoa kwa wanachama unaendelea
kufanyiwa kazi pamoja na suala la pensheni ya pamoja kwa mifuko yote.
Kuhusu nyumba zinazojengwa na mifuko hiyo kuuzwa kwa bei kubwa, Isaka
alisema ni kutokana na utaratibu wa kutumia zabuni wakati wa ujenzi,
lakini aliongeza kuwa baadaye watakuja na mwongozo mbadala ili kutoa
unafuu ambao mwanachama ataweza kukopeshwa kiwanja ajenge mwenyewe.
No comments:
Post a Comment