MKAZI wa Kijiji cha Stalike, wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi,
Thobias Amando (54), ameuawa kwa kushambuliwa na watu wasiofahamika.
Amando aliuawa siku moja baada ya kuwa shahidi katika mauzo ya shamba
kati ya muuzaji, Sadoti Tende na mnunuzi, Gasper Damian. Shughuli ya
mauziano ya shamba hilo ilifanyika nyumbani kwa Gasper.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la polisi wa Mkoa wa Katavi, Emmanuel Nley,
alisema mauaji hayo yalitokea usiku wa kuamkia juzi kijijini hapo.
“Siku moja kabla ya tukio marehemu alifuatwa nyumbani kwake na
jirani yake ili akawe shahidi katika mauziano ya shamba kati ya
Sadoti Tende ambaye alikuwa muuzaji na Gasper Damian kama mnunuzi wa
shamba hilo, mauziano hayo yalifanyika nyumbani kwa Gasper Damian,”
alisema.
Baada ya hapo marehemu hakurejea nyumbani kwake hadi kesho yake
majira ya saa tano asubuhi ambapo mkewe, Magreth Kaombwe, aliamua
kwenda kumfuatilia nyumbani kwa Gasper baada ya kuona mumewe
hajaonekana nyumbani,” alisema kamanda huyo wa Polisi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mke huyo wa marehemu alipofika nyumbani
kwa Gasper alimkuta na alipomuuliza mumewe yuko wapi, Gasper alijibu
tangu walipoachana jana baada ya kumaliza shughuli ya kuuza shamba
hajaonana naye.
Alisema mwili wa marehemu ulikutwa kichakani na watu wawili
waliohusika na mauzo ya shamba hilo, Gasper na Damian wanashikiliwa
na polisi.
No comments:
Post a Comment