WAKATI mataifa mbalimbali duniani yakipambana kukomesha biashara
haramu ya kuuza watu, imeelezwa kuwa ni ya pili kwa ukubwa duniani
kufanyika baada ya dawa za kulevya, huku zaidi ya watu laki 6 kutoka
Afrika wakiwa waathirika wakubwa.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Madawa ya
Kulevya na Uhalifu (UNODC), zinazoeleza kuwa wafanyabiashara wamekuwa
wakijipatia kiasi cha dola bilioni 31 kwa mwaka na kwamba hadi kufika
mwaka 2011 watu milioni 2.5 duniani kote walishauzwa.
Katika mahojiano maalum na Tanzania Daima, Msemaji wa Shirika la
Uhamiaji Duniani (IOM), Jumbe Omar Jumbe, alisema katika biashara hiyo
nchi ya Ukraine na zile za Uarabuni ndizo zinazoongoza.
Aliongeza kuwa watu wanaofanya biashara hiyo kutoka nchi hizo wamekuwa wakiwakusanya watu na kuwauza katika maeneo mbalimbali.
Katika Afrika, Jumbe alisema nchi zinazojishughulisha zaidi na
biashara hiyo ni Morocco, Sudan na Uganda huku akibainisha kuwa tatizo
hilo limekuwa gumu kugundulika Tanzania kwa kile alichoeleza kuwa
matajiri wa biashara hiyo wanakaa nchi za nje na kuwatumia mawakala
kufanikisha shughuli zao.
Jumbe alitaja sababu za watu kukubali kuuzwa kuwa ni pamoja na tamaa
ya kutafuta maisha bora na kubainisha kuwa wengi wanaofikishwa katika
maeneo waliyouzwa wanakuta mambo ndivyo sivyo na kutaja kundi
linaloathirika kwa kiasi kikubwa kuwa ni la wanawake.
Alisema imekuwa ngumu kukomesha biashara hiyo kutokana na
wafanyabiashara hiyo kuwa na fedha nyingi wanazotumia kuwahonga
watumishi wasio waaminifu kufanikisha mbinu zao.
Hivi karibuni Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi Duniani (UNHCR)
kwa kushirikiana na IOM, liliandaa semina ya siku mbili ya kuwajengea
uwezo waandishi wa habari kuhusu masuala ya wakimbizi na wahamiaji,
iliyofanyika jijini Dar es Salaam huku biashara ya binadamu ikiwa moja
ya mada zilizojadiliwa.
Ofisa Mwandamizi wa UNHCR, Edmond Kamina, alisema lengo la semina hiyo
ni kujenga mahusiano ya karibu na mashirika hayo na kuwajengea uwezo
waandishi kuandika kuhusu masuala hayo.
No comments:
Post a Comment