UNAWEZA ukacheka, lakini ndio ukweli. Kocha, ambaye viongozi wa
Simba hawataki kusikia japo jina lake likitajwa Patrick Liewig ametamka
kwamba ; “Nakuja Dar es Salaam dakika yoyote.”
Kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika alipigwa chini na Simba na tayari mrithi wake Abdallah Kibadeni ameshaanza kazi kwenye Uwanja wa Kinesi jijini Dar es Salaam.
Mkataba wa Liewig ulikuwa unamalizika mwisho wa
mwezi huu na Mwanaspoti linajua Simba tayari wana barua yake ya
kumwachisha kazi ingawa hawajamtumia.

Liewig aliliambia Mwanaspoti juzi Jumapili usiku kwamba; “Nakuja Dar es Salaam muda wowote kuanzia sasa kuna taratibu zangu nyingi sana hazijafuatwa, kitaeleweka nikifika huko huko. Nataka kuja kukaa meza moja na Mwenyekiti (Ismail Aden Rage) pamoja na Hanspope (Zacharia).
“Mimi ni profesheno na nina uzoefu na soka la Afrika, siwezi kukimbilia kwenye mambo ya sheria kwanza, ngoja nikae nao tukishindwa kuelewana ndio hatua nyingine zifuate.”
Simba hawataki hata kumsikia kocha huyo wa
Ufaransa na wamekuwa wakitoa kauli tofauti kuhusu kumwachisha kazi
ingawa Mwanaspoti linajua kuwa wameshindwa kutokana na mshahara wa dola
6,000 kudaiwa kuwa ni mkubwa mno.
Kwa kipindi kifupi alichokuwapo Simba, Liewig
alileta nidhamu ya hali ya juu ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha nyota wa
timu hiyo kama Haruna Moshi na Juma Nyosso.
No comments:
Post a Comment