Rais Dk. Jakaya Kikwete amesema viongozi wa dini ndiyo wanaoweza kuwaongoza waumini wao katika maisha ya amani na utulivu.
Amesema serikali inategemea mchango wao katika kuidumisha nchi katika hali hiyo.
Dk Kikwete alisema hayo mjini hapa baada
ya maadhimisho ya ibada ya misa takatifu ya Jubilee ya miaka 25 ya
Mhashamu Askofu Telesphori Mkude wa jimbo Katoliki la Morogoro.
Maadhimisho yalifanyika katika viwanja vya
shule ya sekondari ya St Peter na kuhudhuriwa na maaskofu wa majimbo
yote Tanzania bara na visiwani, waumini na wageni.
Aliwataka viongozi wa Kanisa Katoliki
kuendelea kuwalea vijana katika maadili mema yanayompendeza Mwenyezi
Mungu na kudumisha amani, utulivu, upendo na mshikamano ili taifa
lisiangamie.
Alimpongeza Askofu Mkude kwa jitihada
mbalimbali anazofanya katika kuboresha huduma za afya na elimu katika
jimbo hilo hali inayosaidia jitihada za serikali za kupunguza vifo vya
mama na mtoto.
“Serikali inatambua mchango unaofanywa na
kanisa Katoliki katika kuleta maendeleo ya nchi hasa katika kuchangia
huduma mbalimbali za kijamii, kama elimu na afya na Serikali itaendelea
kuunga mkono jitihada hizo,” alisema Dk. Kikwete.
Naye Askofu Mkude akishukuru alisema kuwa
gharama ya wito ni uaminifu na uadilifu ndani na nje ya kanisa na hata
walioko katika ndoa, na wengine waliopewa dhamana mbalimbali katika
maisha ya binadamu wanapaswa kuzingatia misingi hiyo.
Alisema kwa miaka mingi kuanzia familia
zao, wao wenyewe na vizazi kwa vizazi wamekuwa wakichanganyika Wakristu
kwa Waislam bila kujali matabaka ya kiimani, hivyo inashangaza kuona kwa
siku za karibuni fujo na mambo mengine yenye itikadi za kiimani kama
kuchinja yameanza kusababisha ugomvi.
“Mbona hatugombaniani makaburi wala
kuzika? kuna nini kwenye kuchinja kuna malipo fulani mbona toka zamani
tulikuwa tunafanya na hatukufika huko, siyo sahihi kwa mkuu wa mkoa wala
wa wilaya kubainisha nani ana haki ya kuchinja, hilo sio jukumu lake,
kwani haliko kwenye katiba ya nchi, mipaka inafaa kujulikana na
tukielekezana hatugombani,” alisisitiza Askofu Mkude.
Askofu Mkude alitoa wito kwa Serikali
kuwadhibiti watu kutoka nchi nyingine ambao wanaonekana kufika nchini na
kusababisha baadhi ya vurugu zinazojitokeza.
Awali kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini,
Mwadhama Cardinali, Polycarp Pengo, alisema mara nyingi binadamu
wamekuwa wakijisahau pindi wanapokumbana na matusi na dharau na kumuweka
Yesu pembeni na kuanza kuhangaika, mambo ambayo hayapaswi kufanywa na
Mkristo wa kweli.
Alisema ili wafanikiwe safari yao ya kiroho na kimaisha ni vyema wakamtanguliza Mungu kwa kila jambo.
Alisema kuwa nafasi ya jubilee kwa Mkristo
ni wakati wa kudhihirisha imani na kumwomba Mungu radhi kwa yale
yaliyowateteresha kipindi cha nyuma na kuanza maisha mapya yaliotukuka.
Naye Msaidizi wa Askofu jimbo Katoliki la
Morogoro Padre, Patric Kung’alo alisema kuwa umoja wa mapadri jimbo la
Morogoro umechanga kiasi cha Sh. 7,890,000 kwa ajili ya kuzindua mfuko
wa bima ya afya wa AAR wa Nairobi nchini Kenya utakaotumika kutoa
matibabu kwa Askofu wa jimbo Katoliki la Morogoro Telesphori Mkude.
Fr Kung’alo alisema kuwa mfuko huo pia
utatumika kwa malipo ya Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) kwa kadi ya kijani
kwa mapadri 25 wa jimbo hilo na kwamba waumini wa jimbo hilo wamempatia
askofu Mkude zawadi ya Shilingi milioni 25 pamoja na magurudumu matano
ya gari yaliotolewa na umoja huo wa mapadri.
No comments:
Post a Comment