Chama cha Wananchi (CUF), kimeandaa maandamano ya amani Jumamosi
ijayo kuelekea Ikulu kwa lengo la kumfikishia malalamiko Rais Jakaya
Kikwete, kuhusu vitendo vya ukatili vinavyofanywa na jeshi la polisi na
JWTZ huko Mtwara.
Pia maandamano hayo yamelenga kumtaka Rais
kuhakikisha kuwa ripoti ya uchunguzi ya maafa ya mlipuko wa bomu kule
Arusha inawekwa wazi na wahusika wote wanachukuliwa hatua stahiki.
Naibu Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi na
Siasa wa chama hicho, Shaweji Mketo, aliyasema hayo jana jijini Dar es
Salaam na kuongeza kuwa, maandamano hayo hata kama ikitokea jeshi la
polisi ikayazuia, yatafanyika kama yalivyopangwa.
Akielezea kuhusu maandamano hayo, Mketo
alisema kuwa, tayari wameshamwandikia barua Rais na jeshi la polisi
kuhusu azma hiyo na kwamba Ikulu wanatarajia kupokelewa na
Kikwete au
mwakilishi wake. Alisema Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Suleman Kova, amempigia simu muda mfupi kabla ya kuzungumza na
wanahabari na kumtaka aende Polisi Kati kwa ajili ya kuandaa njia za
kupita siku hiyo.
Alisema maandamano hayo yataanza saa 4:00
asubuhi eneo la Buguruni kituo cha mafuta kuelekea Barabara ya Uhuru,
Mnazi Mmoja, Bibi Titi, Posta Mpya, Ardhi na hatimaye Ikulu.
Kuhusu Mtwara, Mketo alisema wanataka
kumfikishia Rais malalamiko ya wananchi wa Mtwara kutokana na vitendo
vya ukatili vinavyofanywa na polisi na Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ).
Pia alisema maandamano hayo yamelenga
kuishinikiza serikali kukomesha vitendo vya kinyama, kijangili
vinavyofanywa na majeshi hayo kwa kuwakamata, kuwatesa na kuwabaka
wananchi wasio na hatia mkoani humo.
No comments:
Post a Comment