KATIKA mwendelezo wa kuibana CHADEMA, Mbunge wa Mbeya Mjini,
Joseph Mbilinyi ameshikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma jana kwa
mahojiano ya saa tatu akidaiwa kuandika ujumbe wa kumkashifu Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda.
Mbilinyi maarufu kama Sugu anadaiwa kusambaza ujumbe huo kwenye
mtandao wa kijamii ukisomeka; “Tanzania haijawahi kuwa na Waziri Mkuu
mpumbavu kama Pinda.”
Akithibitisha kuhojiwa kwa mbunge huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Dodoma, David Misime alisema walimshikilia kuanzia saa 8 mchana hadi
10:30 jioni na kisha kumwachia kwa dhamana.
Misime alisema Mbilinyi atatakiwa kuripoti polisi leo asubuhi na kwamba uchunguzi wa tukio hilo ulikuwa ukiendelea.
Mbilinyi anadaiwa kuandika maneno hayo kwenye ukurasa wake wa
facebook baada ya Pinda kusema watu wanaokaidi amri ya polisi wapigwe
tu, akiitafsiri kauli hiyo kuwa ni upumbavu.
Alipotafutwa na Tanzania Daima Jumatano kuzungumzia tukio hilo,
Mbilinyi hakupokea simu yake ya kiganjani ingawa Mkurugenzi wa
Mawasiliano na Habari wa CHADEMA, John Mnyika alithibitisha kuwa
alipewa dhamana.
Wiki iliyopita katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri
Mkuu, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza
Mangungu kuhusu kauli ya serikali katika vurugu zenazoendelea nchini,
Pinda alisema wanaokiuka amri wapigwe tu na polisi.
Alifafanua kuwa anasema wapigwe kwa kuwa serikali imechoka na vitendo
vya vurugu. “…Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna
nyingine…maana tumechoka.”
Kombati za CHADEMA mzozo
Siku moja baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
Freeman Mbowe na wabunge wenzake watatu kuzuiwa kuingia bungeni juzi,
uongozi wa Bunge umesisitiza kuwa kombati zao zinakiuka kanuni.
Mbowe na wabunge wenzake wa CHADEMA, Tundu Lissu (Singida Mashariki),
Godbless Lema (Arusha Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana) walizuiwa na
askari kwa madai kuwa wamevalia sare za chama ambazo kikanuni
haziruhusiwi.
Uamuzi huo uliibua hali ya sintofahamu kwa wabunge wa CHADEMA
kutokana na Mbowe kuvalia vazi hilo mara nyingi tangu aingie bungeni
mwaka 2010.
Licha ya kanuni za Bunge kuruhusu vazi la ‘safari suti’ kwa wanaume
lenye mshono kama kombati zinazovaliwa na baadhi ya wabunge wa CHADEMA,
Tanzania Daima Jumatano limebaini kuwa uamuzi huo unaacha maswali
mengi yanayohitaji majibu.
Akizungumzia uamuzi huo jana, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John
Joel alisema suti hizo za wabunge wa CHADEMA zilikiuka kanuni ya 149
(3) (b) (i).
Kipengele hicho cha kanuni kinasomeka kuwa inaruhusiwa suti ya
Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya
mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani, ya rangi moja, isiyokuwa
na nakshi, pamoja au bila baragashia.
Joel alifafanua kuwa yawezekana huko nyuma wamekuwa wakifanya makosa
kwa kuwaruhusu wabunge hao kuingia na suti hizo, lakini sasa kuanzia
juzi wameamua kuanza
kuchukua hatua ya kuwazuia.
“Zile wanasema sio sare ya chama, lakini wote tunawaona kwenye
mikutano na shughuli za chama ndizo zinavaliwa na isitoshe tuliwahi
kuwatahadharisha kuwa ziko kinyume na kanuni wasizivalie bungeni ila
wamekuwa wakiendelea kuzivaa,” alisema.
Licha ya kanuni hiyo kuwa kimya kuhusu kuvaa sare za vyama bungeni,
Joel alisema kuwa uamuzi huo ulikuwa ni busara ya spika wa wakati huo,
Samuel Sitta, lakini haujaingizwa kwenye kanuni kimaandishi.
Tanzania Daima Jumatano lilitaka kufahamu ni kwanini uamuzi huo
ukaanza ghafla juzi baada ya wabunge wa CHADEMA kurejea kutoka jijini
Arusha, na Joel bila kufafanua alisema: “Kawaulize walipanga nini
wakiwa Arusha? Ndiyo maana tukaamua kuchukua hatua.
“Bora tukaonekana tumewaonea kuliko kuendelea kufumbia macho kanuni.
Tuwe wawazi kombati zao zina nakshi kupitiliza kwa mujibu wa kanuni.
Kwanini wakina Halima Mdee na Vicent Nyerere tuliwaacha wakaingia?
Mbona kombati za Zitto zinatofautiana na wengine?”
Alipotakiwa kufafanua kama kweli walishaonywa wasivae kombati hizo
bungeni,
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari wa CHADEMA, John Mnyika
alisema Joel hajui kanuni za Bunge ndiyo maana amekuwa anampotosha
spika na viongozi wa Bunge kufanya uamuzi wa ajabu.
“Wametuzuia juzi kwa sababu ya maelezo ya akina Pinda na Serikali ya
CCM, sio kwa sababu ya ukiukwaji wa kanuni za Bunge. Kumekuwa na
utamaduni wa hovyo wa kutafsiri vibaya kanuni za Bunge kwa lengo moja
tu, kuwadhibiti CHADEMA,” alisema.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alitolea mfano akisema kuwa
walizuiliwa kuingia ukumbini na askari polisi wasiokuwa na mamlaka ya
kuwazuia kuingia ndani bali walitakiwa wasubiri amri ya spika kuwatoa
ukumbini ndipo wawatoe.
“Hayo yote hawezi Joel kufahamu, anafanyia uzoefu alioupata wakati
anafanya kazi Makao Makuu ya CCM wakati wa Bunge la chama kimoja,”
alisema Mnyika.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Lissu ambaye pia ni Mnadhimu
wa kambi ya upinzani bungeni, alisema kuwa walishangazwa na uamuzi huo
wakati mavazi hayo wamekuwa wakiyavaa miaka yote na kuingia nayo
bungeni.
Lissu alisema kuwa hatua hiyo waliichukulia kama mkakati maalumu wa
Serikali ya CCM kutaka kuwazima kabisa kuhakikisha hawapati nafasi ya
kuingia bungeni ili kujibu tuhuma walizosingiziwa kuhusiana na mlipuko
wa bomu jijini Arusha.
“Sisi hali hiyo tulianza kuishtukia tangu asubuhi tulipoingia kwenye
eneo la Bunge, kama mligundua kulikuwa na askari wengi sana kila kona
kuliko kawaida kana kwamba nchi imepinduliwa. Kinyume na utaratibu wa
kanuni askari wa kawaida wameingizwa hadi bungeni,” alisema.
Hata hivyo, pamoja na uamuzi huo, kanuni za Bunge hakuna mahali
zinazuia mbunge kuvaa sare ya chama chake isipokuwa kanuni zimeainisha
aina za mavazi ya kuvaliwa na wabunge wanawake na wanaume.
Kwa mujibu wa kanuni ya 149 (3)(b) kwa wanaume wanaruhusiwa kuvaa (i)
suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au
shingo ya mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani, ya rangi moja,
isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila baragashia;
(ii) vazi la kimwambao yaani kanzu rasmi na nadhifu, koti,
baraghashia na makubadhi au viatu; (iii) suti kamili ya kimagharibi ya
rangi kadiri isiyomeremeta; (iv) koti aina ya blazer na tai, pamoja na
suruali yoyote ya heshima; au (v) tarbushi na kilemba cha Singasinga,
au kilemba chochote kinachovaliwa kwa mujibu wa masharti ya imani au
mila.
Via Tanzania daima.
No comments:
Post a Comment