WAZIRI Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amesema anashangazwa na
baadhi ya viongozi wa dini kutoa sifa nzuri kwa watu wanaochanga fedha
na si kuzingatia uadilifu na wema walionao.
Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo jana katika sherehe za kutimiza miaka
50 tangu kuanzishwa kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), zilizofanyika katika Chuo Kikuu cha Makumira mkoani Arusha.
Sumaye alihoji kuwa inakuwaje wema wa baadhi ya watu unajitokeza
zaidi wakati nchi ikielekea kwenye uchaguzi unaotegemewa kufanyika
mwaka 2015.
Sherehe hizo za kutimiza miaka 50 zilifanyika katika Chuo Kikuu cha
Makumira na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa KKKT kutoka sehemu
mbalimbali duniani pamoja na maaskofu wote wa dayosisi 20 zilizopo
nchini.
Ingawa Sumaye hakumtaja anayemlenga, lakini inaonekana kumlenga
Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ambaye katika siku za hivi
karibuni amekuwa akimiminiwa sifa kuwa ni mpambanaji wa umasikini na
mtu mzuri katika kuendesha harambee makanisani zinazowezesha
kupatikana mamilioni ya fedha.
Hivi sasa, Lowassa anaonekana ndiye ‘mtaji’ mkubwa kwa viongozi wa
makanisa yanayohitaji kuendeleza miradi mbalimbali ambapo wamekuwa
wakimualika kwenye harambee zao.
Lowassa mwenyewe alikaririwa hivi karibuni mkoani Dodoma akisema kuwa
yeye hana mamilioni ya fedha kama baadhi ya watu wanavyomhusisha
anaposhiriki harambee, bali ana watu wenye ushawishi katika jamii.
Kauli ya Sumaye
Sumaye alisema ni jambo la kutia aibu na kushtua kuona watu wakipewa
sifa za kuvutia kwa sababu ya kuchangia mamilioni kwenye shughuli za
kanisa au binafsi na si kwa sababu ya uadilifu au wema wao.
Alisema katika siku za hivi karibuni kumeibuka mambo mengi machafu
yaliyokithiri katika jamii na watu wanyonge kukosa haki zao za msingi
hadi watoe hongo au rushwa.
“Nafasi katika nchi zimekuwa za biashara, watu hawaangalii tena uwezo
au uadilifu wa mtu anayeutaka uongozi bali wanaangalia ametoa fedha
kiasi gani za kuwahonga wapiga kura.
“Hata katika baadhi ya dayosisi zetu na sharika zetu watu wakipewa
sifa za ajabu si kwa sababu ya uadilifu wao au wema wao, bali kwa
sababu tu wamechangia fedha kwa shughuli zetu za kanisa au hata
binafsi.
“Hatujiulizi kuwa mbona wema huu unajitokeza zaidi wakati kama kuna
uchaguzi unaotegemewa? Je, hapo hatusatahili kutupwa nje na kukanyagwa
kanyagwa kwa sababu chumvi imepotea utamu wake?
“Je, haya ni mafanikio ya miaka 50 ya kanisa au ni maeneo ambayo inabidi tujitazame na tujirekebishe?” alihoji.
Kuhusu kanisa hususani masuala ya kijamii, Sumaye alisema pamoja
kushughulikia masuala ya kiroho, bado linapaswa kushughulikia masuala
ya mwili ambao ni hekalu la Mungu, hivyo kanisa lina jukumu kujenga
jamii yenye maadili mema na kukemea maadili mabaya.
“Yesu alisema; ‘nyinyi ni chumvi ya ulimwengu’, lakini chumvi ikiwa
imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena ni ya kutupwa nje
ikinyagwe na watu.
“Lakini nasema nyinyi ni nuru ya ulimwengu, hivyo ni wajibu wenu
kutoa nuru kwa wengine maana yake ni kutoa malezi mema kwa jamii. Je,
kanisa letu limefanikiwa kwa kiasi gani katika eneo hili?
“Je, tumekuwa na ujasiri wa kukemea mabaya hata kama kukemea huko
kunawaudhi au kuwakera wenye mamlaka au na wenye nguvu za fedha? Je,
tuna ujasiri kama wa Nabii Mikaya mwana Imla, aliyemwambia mfalme wake
nitasema yake bwana aliyoniambia na kumwambia mfalme kuwa ukienda
kupigana vita vya kuteka Tamoth Gileadi hutarudi hai?” alihoji Sumaye.
Sumaye pia alizungumzia matukio yaliyoanza kujitokeza katika siku za
hivi karibuni akisema hivi sasa taifa limekuwa na matatizo mengi ya
watu kuchukiana kwa sababu ya imani zao, mabomu kulipuliwa katika
mikusanyiko ya jamii na kuteketeza watu wasio na hatia.
“Leo Watanzania wanabaguana kwa maeneo wanakotoka na sababu nyingine
zisizo na msingi, matukio ya viongozi wa dini kuuawa, uchomaji moto wa
makanisa, mapigano ya nani achinje mnyama, haya yote ni mambo mageni
nchini mwetu, tuendelee kuimboea nchi yetu amani, lakini wakati maombi
yakiendelea Watanzania tujue tunajichimbia kaburi letu wenyewe kama
hatutapiga vita maovu haya,” alisema Sumaye.
Naye Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini, Askofu Dk. Alex
Malasusa, alisema kanisa halitaogopa hujuma au kusema ukweli na
wataendelea kujenga marafiki wema bila kujali itikadi za marafiki wao.
Katika hatua nyingine, Askofu Malasusa alibainisha kuwa kitendo cha
viongozi dini ya Kiislamu kuhudhuria sherehe hizo za miaka 50
kimeonyesha sura mpya.
“Kuwapo kwa viongozi wa dini ya Kiislamu kumedhihirisha kuwa yanayozungumzwa nje si halisi,” alisema Dk. Malasusa.
Katika sherehe hizo maaskofu wa kanisa hilo walihudhuria ikiwamo pia viongozi kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Via Tanzania daima
No comments:
Post a Comment