KIUNGO mahiri wa Simba na timu ya soka ya Tanzania, Taifa
Stars, Amri Kiemba, juzi alitwaa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka katika
hafla iliyofanyika chini ya uratibu wa Umoja wa Wanasoka Tanzania
(Sputanza), kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Mbali ya Kiemba, mchezaji Salum Abubakar ‘Sure boy’ wa Azam FC
alitwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi wa mwaka, huku Kocha wa Mtibwa
Sugar ya Turiani, Morogoro, Mecky Maxime akibeba tuzo ya Kocha Bora
huku kipa bora akiwa ni Hussein Sharif, pia wa Mtibwa.
Tuzo hiyo iliyofanyika kwa mara ya kwanza kwa lengo la kuongeza
ushindani kwa wachezaji kwenye klabu zao na timu za taifa, imefanyika
chini ya udhamini wa Kampuni ya Kishen Enterprises Ltd katika vigezo
vya nyota bora wa mwaka, chipukizi bora na kocha bora na kipa bora.
Kiemba aliibuka mshindi wa tuzo hiyo akiwabwaga Haruna Niyonzima,
Didier Kavumbagu wote wa Yanga, Kipre Tchetche (Azam FC) na
mshambuliaji Paul Nonga wa JKT Oljoro.
Kwa upande wa Sure boy, alitwaa tuzo yake akiwabwaga Hassan Dilunga
wa Ruvu Shooting, Idrisa Rashid wa Yanga, Frank Sekula na Shomari
Kapombe wa Simba.
Mexime alijitwisha tuzo akiwashinda Charles Boniface Mkwasa wa Ruvu
Shooting, Abdallah Kibadeni wa Kagera Sugar na Jumanne Chale wa
Tanzania Prisons. Sharif aliwashinda kipa namba moja wa Simba na Stars,
Juma Kaseja na Mwadin Ally wa Azam FC.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Sputanza, Musa Kisoki
alisema washindi wa tuzo hizo wamepatikana baada ya uteuzi na upigwaji
kura uliofanywa na makocha na manahodha wa timu mbalimbali nchini.
Alisema vigezo vilivyotumiwa ni sifa ya mchezaji, nidhamu ya ndani na
nje ya uwanja, mafanikio yake kwenye klabu yake, uwezo wake binafsi na
mambo mengine yanayofanana na hayo na akawashukuru wote walioshiriki
kwa namna mbalimbali kufanikisha tuzo hiyo.
“Nawashukuru waliofanikisha tuzo hizi na wote mliofika kwani huu ni
mwazo, lakini naamini tutafikia mafanikio makubwa katika maandalizi
mengine badae yanayokuja kwa kuwa kila jambo huwa gumu mwanzoni,”
alisema Kisoki.
Alisema tuzo hizo zitakuwa zikitolewa kila mwaka chini ya udhamini wa
Toyo ili kuwaongezea wachezaji na makocha ari uwanjani wakati wa
mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Miongoni mwa viongozi walioshudhuria hafla hiyo ni Mama Salma Kikwete
aliyekabidhi zawadi za pikipiki na vyeti vya kuwakumbuka na
kuwapongeza wachezaji wakongwe wa zamani waliochezea timu ya taifa
miaka ya nyuma.
Naye mgeni rasmi katika tuzo hizo, Makamu wa Rais wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani aliwasihi Sputanza kuwasaidia
wachezaji katika vita ya dawa za kulevya na vitendo vya rushwa kwa
ajili ya kuhujumu timu.
“Nawapongeza wote kwa ujumla wenu kwa heshma hii mliyowapa wachezaji
kwani naamini itakuwa chachu katika kuendeleza mchezo wa soka nchini,”
alisema Nyamlani.
No comments:
Post a Comment