Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema sheria ya kutumia
wachezaji watatu wa kigeni badala ya watano itaanza kutumika msimu wa
2014/15 hivyo msimu ujao wa 2013/14 wachezaji watano wa kigeni
wataendelea kutumika kama kawaida baada ya kupata maombi mengi ya
viongozi wa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa kauli hiyo, sasa klabu za Simba, Yanga na Azam zitapata ahueni kutokana na kuwa na wachezaji wengi wa kigeni.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema sheria ya kutumia wachezaji watatu wa kigeni itaanza kutumika msimu wa 2014/15 na utekelezaji huo utafanyika moja kwa moja bila kuhusisha makubaliano ya viongozi ambao hivi sasa wameomba kusogezwa mbele sheria hiyo.
Angetile alisema awali sheria ya kutumia wachezaji watatu wa kigeni ilitazamiwa kuanza msimu unaokuja wa 2013/14, lakini kutokana na mapendekezo mengi ya viongozi wa klabu, hivi sasa wamesogeza mbele sheria hiyo mpaka msimu wa 2014/15.
“Tulikaa na klabu ili tupate maoni yao, kwa sababu
ilikuwa tuanze mapema tu kutumia sheria hiyo, lakini klabu zimeomba
tuanze kutumia sheria ya kusajili wachezaji watatu wa kigeni msimu wa
2014/2015,”alisema Osiah.
Alisema viongozi wa klabu wameomba sheria hiyo isogezwe mbele kwa sasa ili waweze kumalizana na mikataba ya wachezaji wao wa kigeni kwa hiyo wameamua kuzikubalia klabu hizo za Ligi Kuu.
“Kufuatia mapendekezo mengi ya viongozi wa klabu tumeamua kupeleka mbele sheria hii ya kutumia wachezaji watatu, sheria itaanza rasmi kutumika msimu wa 2014/15, “alisema Osiah.
No comments:
Post a Comment