MEYA wa Manispaa ya Ilemela, Henry Matata, amefunguliwa jalada
polisi akidaiwa kutishia kumuua mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia
(CHADEMA), katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichohudhuriwa na Mkuu
wa Wilaya ya Ilemema, Amina Masenza.
Matata ambaye ni Diwani wa Kata ya Kitangiri aliyevuliwa uanachama wa
CHADEMA mwaka jana kutokana na kusababisha mgogoro ndani ya chama mkoani
Mwanza lakini alifungua kesi mahakamani kupinga uamuzi huo ambapo kesi
hiyo bado inaendelea.
Hata hivyo katika hatua ya kushangaza, Septemba mwaka jana, Matata
alichaguliwa kwenye mkutano ambao ulikuwa haukidhi akidi ya wajumbe
ambao ni madiwani 14 na kwa mujibu wa sheria ndio wanaounda halmashauri
hiyo mpya iliyomegwa kutoka katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini hapa, Kiwia alisema
Matata alimtishia kumuua Julai 26, mwaka huu, katika kikao hicho na
kwamba tayari amefungua jalada polisi mkoa Mwanza kulalamikia vitisho
hivyo.
Kiwia alisema kuwa chanzo cha vitisho hivyo ni msimamo wake wa
kumpinga Meya Matata kuongoza kikao hicho ambapo siku hiyo mbunge huyo
alisimama na kumuomba Mkurugenzi wa Manispaa, Zuberi Mbyana, amteue
mwenyekiti wa muda ili aongoze kikao.
Alisema kuwa alifikia uamuzi huo kutokana na madiwani wa CHADEMA
kutomtambua Matata kama Meya wa Manispaa hiyo wakilalamikia uchaguzi
uliomweka madarakani kuwa ulikuwa batili kwa vile alichaguliwa na
madiwani sita wa CCM na CUF bila kuwepo madiwani wao nane.
“Siku ya kikao niliomba ateuliwe mwenyekiti wa muda aongoze kikao
maana Matata si Meya wa Ilemela kisheria. Baada ya kusema hivyo, Matata
alisimama na kusema angeliniua.
Alirudia kauli yake mara mbili tena
mbele ya mkuu wa wilaya, polisi na wajumbe wengine waliohudhuria kikao
hicho,” alisema.
Kiwia alidai kushangazwa na kitendo cha mkuu wa wilaya ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya pamoja na askari
waliokuwepo kikaoni kunyamazia tukio hilo na kushindwa kumkamata Matata
na kumchukulia hatua.
Alisema kuwa kwa sasa ana mashaka na usalama wa maisha yake kwani
kitendo cha mkuu wa wilaya kushindwa kumchukulia hatua meya huyo kinatia
hofu juu ya usimamizi wa sheria.
“Kwa kweli nashindwa kuelewa utendaji wa mkuu huyu wa wilaya, yaani
mtu anasimama mbele yake na kumtishia mtu maisha halafu yeye na askari
wanakaa kimya tu,” alihoji.
Kiwia aliongeza kuwa baada ya vitisho hivyo, yeye pamoja na madiwani
wenzake wawili wa CHADEMA, Rosemary Brown wa Kata ya Pasiansi na Gradis
Kiwia wa viti maalumu walitoka nje ya kikao huku Matata akitishia
kumfukuza udiwani Brown.
Alipoulizwa jana kuhusu tuhuma hizo za kutishia kumuua Kiwia, Matata
alisema mbunge huyo asiogope kuuawa maana asipomuua yeye atauawa na
wengine endapo hatapunguza mdomo.
Katika hatua nyingine, meya huyo anadaiwa kushikiliwa kwa muda na
Jeshi la Polisi Wilaya ya Ilemela juzi kwa tuhuma za uchochezi.
Matata anadaiwa kuwahamasisha wananchi wa Mhonze kuwapiga mawe maofisa
wa jiji la Mwanza watakapokwenda eneo hilo kugawa viwanja.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, polisi ilimshikilia kwa mahojiano zaidi
kuhusu tuhuma hizo za uchochezi. Matata alikiri kuwaamuru wananchi wa
kijiji cha Mhonze kuwafanya hivyo lakini alikanusha kuhojiwa na polisi
badala yake alisema alikwenda kituoni kwa masuala mengine na si
vinginevyo.
“Kweli niliwaapia wawapige mawe watu wa jiji maana watakwendaje kupima na kugawa viwanja eneo lisilo lao.”
Uchaguzi wa Matata ulikiuka kanuni na sheria za halmashauri. Kwa
mujibu wa sheria ni kwamba akidi ya wajumbe iliyokuwa ikihitajika kwa
ajili ya meya kupigiwa kura ni madiwani tisa badala ya madiwani sita
walioshiriki kwenye uchaguzi huo.
Badala yake Matata alichaguliwa kuwa meya na madiwani sita pekee,
wanne wa CCM na mmoja wa CUF baada ya madiwani wengine wa CHADEMA
kususia mkutano huo wa uchaguzi.
Matata alichaguliwa wakati suala lake la kufukuzwa uanachama ndani ya
CHADEMA likiwa bado linangojea uamuzi wa mahakama alikofungua kesi
kupinga uamuzi wa chama chake.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment