WATU wawili wamefariki dunia akiwemo mwanafunzi wa shule ya
msingi mjini hapa ambaye amejinyonga kwa kamba ya katani hadi kufa kwa
madai ya kunyimwa mhindi na wadogo zake.
Kamanda wa Polisi Tarime na Rorya, Justus Kamugisha alimtaja
mwanafunzi huyo mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake kuwa ni
Richard Charles (14) anayesoma katika Shule ya Msingi St. Jude ambaye
ni mkazi wa Kijiji cha Nyagisya, Kata ya Kiore.
Alisema waligundua mwanafunzi huyo kujinyonga Julai 6 mwaka huu baada
ya kunyimwa mhindi wa kula na wadogo zake, hivyo kushindwa kuvumulia
na kuchukua uamuzi wa kujinyonga kutokana na njaa aliyokuwa nayo.
Kamanda Kamugisha alisema baadaye mwili wake ulichukuliwa na polisi
na kupelekwa katika hospitali ya wilaya ya Tarime kufanyiwa uchunguzi
kisha kukabidhiwa ndugu na jamaa zake kwa ajili ya mazishi, na kwamba
wanaendelea zaidi na upelelezi kuhusu tukio hilo.
Katika tukio jingine, Mtera Chacha (25) mkazi wa Kijiji cha Genkuru
amefariki dunia baada ya kupigwa na kitu chenye ncha kali.
Tukio hilo lilitokea Julai 6 mwaka huu majira ya saa 6.00 mchana
katika Kitongoji cha Nyabigena, Kijiji cha Kewanja, Kata ya Kemambo.
Chanzo kilitajwa kuwa ni Chacha kulisha mifugo katika shamba la mzee
Mwita Mabya (83), na polisi wanaendelea kumuhoji aliyesababisha tukio
hilo.
Katika tukio jingine, Mkwaya Mwita (48) mkazi wa Kijiji cha Gibaso
amekatwa panga kiganjani hadi kutenganishwa na mkono wake na Marwa
Mwita wa Kijiji cha Gibaso.
Kamanda Kamugisha alisema tukio hilo lilitokea jana na kwamba chanzo chake kinadaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Alisema majeruhi amelazwa katika hospitali ya serikali ya wilaya ya Tarime akipatiwa matibabu.
Pia Emmanuel Mseti (19) mkazi wa Kijiji cha Kegonga amejeruhiwa kwa risasi na askari wa hifadhi ya taifa ya Serengeti.
Kamanda Kamugisha alisema kuwa mtu huyo alijeruhiwa kwa risasi katika
kiwiko cha mkono wake baada ya kudaiwa kuingiza mifugo katika hifadhi
hiyo ya taifa na kwamba hivi sasa amelazwa hospitali ya Bugando
akipatiwa matibabu.
No comments:
Post a Comment