JINA la Aunt Ezekiel siyo geni kwa
wadau mbalimbali wa burudani hapa nchini, ni staa ambaye hivi sasa ana
jina kubwa kupitia sanaa yake ya uigizaji wa filamu aliyoianza miaka
sita iliyopita.
Japokuwa kwa sasa ni staa, amepitia mambo mengi magumu katika safari yake ya maisha mpaka kufikia hapo alipo hivi sasa.
Aunt alizaliwa mwaka 1988 mkoani Dar es Salaam, baba yake akijulikana
kama Ezekiel Grayson’ Jujuman’ ambaye alikuwa ni mchezaji hodari sana wa
timu ya Simba. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Bunge mwaka
1993 hadi 1998. Alienda kumalizia darasa la saba katika Shule ya Msingi
Chanzige iliyopo Kisarawe, mkoani Pwani.
Vipi maisha yalikuwaje baada ya kumaliza shule?
“Kwa kweli maisha yalikuwa ni magumu mno kwa maana nilipomaliza shule
tu, alijitokeza mwanaume na kutaka kunioa kitu ambacho mimi sikukipenda
kabisa lakini baba yangu alitaka hivyo kwa vile uwezo wa kunisomesha
hakuwa nao tena na maisha yalikuwa ni magumu sana.
“Baada ya kuona mambo ya mimi kuolewa yanapamba moto huku yule mwanaume
akizidi kuihudumia familia yangu, nikaona nikichelewa nitabebwa
mzobemzobe, hivyo niliamua kutoroka alfajiri na mpaka natoroka, sikuwa
najua naelekea wapi.
“Baada ya kutoroka, asubuhi ile nilienda mpaka Ukonga, sehemu moja
inaitwa Mazizini, nikagonga nyumba moja ya mtu na kumwambia natafuta
kazi za ndani, bila kuchelewa yule dada aliniambia hata yeye anatafuta
msichana, hivyo nilianza kufanya kazi nikawa namlea mtoto na kufanya
kazi zote za ndani huku nyumbani kwetu wakinitafuta bila mafanikio.
“Baada ya kufanya kazi kwa muda wa miezi mitatu, niliamua kumpigia simu
baba yangu ambapo aliposikia sauti yangu alifurahi sana na kuniambia
kuwa nirudi nyumbani wala hawataweza kuniozesha tena, hivyo niliamua
kumuaga tajiri wangu na kumwambia narudi nyumbani kwetu.
“Niliporudi nyumbani bado nilimkuta yule mchumba lakini nilimwambia kama
anataka kunioa anisubiri nisome, hivyo nilienda Iringa katika Shule ya
Sekondari Kawawa na kuanza kidato cha kwanza mpaka cha pili, nikarudi
Dar na kumalizia katika Shule ya Sekondari Makongo mwaka 2004.
“Baada ya kumaliza sekondari, nilijiunga na mambo ya computer pale
Amana, lakini baadaye niliamua kushiriki mambo ya urembo ambapo
niliibuka kuwa Miss Mwanza 2006 na kuingia katika shindano la kumsaka
mrembo wa Tanzania lakini sikufanya vizuri na hapo ndipo nilipoingia
kwenye uigizaji wa filamu ambapo filamu yangu ya kwanza kabisa ilikuwa
ni Miss Bongo, iliyokuwa ya William Mtitu.
“Ilipofika mwaka 2007 nilifunga ndoa ya bomani na mfanyabiashara maarufu
Jack Pemba. Yule mchumba aliyekuwa akinisubiri mwanzo alikuwa
ameshakata tamaa na kuendelea na maisha yake, hivyo nilianza kuishi na
Jack kama mke na mume huku akinisaidia katika mambo yangu ya sanaa.
“Baadaye alinizuia kwani alikuwa hapendi nitoke nyumbani na baada ya
muda nilipata ujauzito wake kitu ambacho kilimfurahisha sana na
kunizawadia vito vya dhahabu vyenye uzito wa kilo moja, lakini kwa
bahati mbaya ilipofika miezi saba nilijifungua mtoto akafariki.
“Ndoa ilikuwa ni nzuri, nilikuwa napata kila kitu ambacho nataka na
kutembelea gari za kifahari lakini kitu ambacho nilikishindwa ndani ya
ndoa hiyo ni kipigo kikali nilichokuwa nakipata, kwani nakumbuka kuna
siku alinipiga kiasi ambacho mashuka meupe yalikuwa kama yamepakwa rangi
nyekundu, hivyo bibi yangu alikuja kunichukua na kuondoka moja kwa
moja.
“Baada ya kuondoka kwa Jack, nilianza kupigana katika maisha na
niliingia kwenye uhusiano na mtu mwingine na nikaanza kuingia kwenye
kucheza filamu ambapo huko jina langu lilizidi kukua siku hadi siku,
hivyo nikawa naweza kuyaendesha maisha yangu ya kila siku, mpaka
nilipokutana na mume wangu wa sasa, Sunday Demonte ambaye alinioa
mwishoni mwa mwaka jana.
“Unajua kazi yangu kubwa mimi ni uigizaji ambapo huku Tanzania ndiyo
kila kitu, sasa nikisema nikae Dubai muda wote ni lazima kipaji changu
kitapotea, hivyo nafanya kazi zangu kwa kutengeneza filamu kama tatu,
kisha narudi Dubai kidogo kukaa na mume wangu.
“Siku zote naumia sana kuwapoteza wazazi wangu wawili, yaani baba na
mama, nilitamani sana mpaka leo wawepo na waione kazi yangu na
nilifurahi sana siku ambayo nilifunga ndoa yangu ya pili na Sunday
Demonte,” anaeleza Aunt.
Credit: Habari Mpasuko Blog
No comments:
Post a Comment