MAUAJI ya bilionea ambaye ni mfanyabiashara mkubwa wa madini ya
Tanzanite huko Mererani mkoani Arusha, Erasto Msuya aliyeuawa kwa
kumiminiwa risasi kibao juzi, yamesababisha kutanda kwa hofu jijini
hapa.
Mwili wa Msuya ukiwa ndani ya difenda.
Tukio hilo lililojiri maeneo ya KIA alipokuwa akitokea Mererani
kuelekea Moshi, Kilimanjaro limeacha maswali mengi ambayo yanahitaji
majibu.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa, bilionea huyo
anayemiliki Hoteli ya SG Resort iliyopo Sakina jijini hapa alipigiwa
simu akielezwa kuwa kuna biashara ya kufanya Moshi lakini kabla ya
kufika alivamiwa njiani.
Ilidaiwa kuwa Erasto aliuawa akiwa na gari lake jipya aina ya Range
Rover Voque la 2013 alilonunua hivi karibu kwa dola za Kimarekani
250,000 (zaidi ya Sh. milioni 400 za Kitanzania).
Wanausalama wakiubeba mwili wa marehemu Msuya.
Habari za kiuchunguzi zilibaini kuwa kuna vitu vingi nyuma ya mauaji hayo huku suala visasi vya kibiashara likipewa kipaumbele.
“Kuna
jamaa mwingine aliuawa juzikati kule Mererani, walikuwa wakifanya
biashara na Erasto hivyo inawezekana ikawa ni kisasi katika mambo ya
biashara ya madini.
“Unajua hii biashara ni ya kuvizianaviziana sana kwa hiyo itakuwa ni
njama kwa sababu kuna watu wanadai wakati anaondoka Mererani alikuwa
ameshanunua mzigo mkubwa.
“Pia inawezekana kweli ni majambazi ambao walijua kabisa Erasto ana mzigo ndiyo maana wakamfanyizia na kuchukua mzigo.
“Hii
inaonesha kuna aina fulani ya utekaji na majibizano ya risasi kwa
sababu tukio lenyewe limefanyika nje ya barabara, porini kabisa na gari
linaonekana limepaki kwa utaratibu wa kawaida bila vurugu ‘so’ kwa
vyovyote ni ishu iliyopangwa,” alisema mmoja wa wafanyabiashara wa
madini aliyefika eneo la tukio.
Uchunguzi mwingine uliibuka na madai kuwa huenda kuna visasi vya
kimapenzi lakini kuvizungumzia inakuwa ngumu kwa sababu ya kukosekana
kwa ushahidi wa moja kwa moja.
“Mimi nakwambia tusubiri, mauaji haya yataibua mambo mengi sana kwa
sababu ndani ya kipindi kifupi kumetokea vifo vya vijana matajiri wenye
umri mdogo kati ya 37 na 40.
“Ukihesabu sasa hivi wanafika matajiri kama watano na wote walikuwa ni ‘kampani’ moja.
“Alianza
Wakili Mawala aliyejirusha gorofani Nairobi, Kenya. Akafuatia Henry
Nyiti, akaja Babu Sameke, akafuatia yule jamaa aliyejirusha gorofani
Kariakoo na yule mwingine aliyepigwa risasi kule Masaki, Dar.
“Sasa Erasto naye ameuawa. Kwa vyovyote kuna kitu. Kama siyo mambo ya
kulogana, basi kuna kitu waligusa,” alisema jamaa mwingine anayewajua
vizuri wafanyabiashara wa madini Arusha.
Habari zinadai kuwa baadhi ya matajiri wamepanga kulikimbia jiji hilo kutokana na hofu juu ya maisha yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alipotafutwa na gazeti hili, simu yake iliita bila kupokelewa.



No comments:
Post a Comment