MBUNGE wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile (CCM), amewatahadharisha
wakazi wa Mbagala Kuu kuepukana na watu wanaopita katika maeneo yao na
kuchangisha sh 1,000 kwa kila mkazi kwa madai watawasaidia kupata haki
zao juu ya fidia ya mabomu.
Ndugulile alitoa kauli hiyo juzi alipozungumza na wakazi wa mtaa wa
Kichemchem, Kata ya Mbagala Kuu, Dar es Salaam na kusema watu hao
wanafanya utapeli wa dhahiri kwa watu wenye matatizo.
Alisema zoezi la uthamini wa ulipaji fidia kwa wahanga wa mabomu ya
Mbagala limemalizika na kwamba wale waliofanyiwa tathmini na majina yao
yakashindwa kuonekana katika kumbukumbu za malipo wanapaswa wawasiliane
na ofisi ya mbunge kwa hatua zaidi.
“Vipo vikundi vinapita na kusema wapo karibu na Waziri Mkuu mara Rais,
nawaambieni hao ni matapeli hakuna uthamini mwingine baada ya ule wa
mwisho kumalizika,” alisema Ndugulile.
Kuhusu ulinzi mbunge huyo alisema ni wajibu wa kila mwananchi kukataa
uhalifu na kuwafichua popote walipo badala ya kusubiri vyombo vya dola
kufanya kazi hiyo.
“Kuna vijana 600 wanapata mafunzo ya polisi jamii; hawa watakuwa na
mafunzo ya ukamataji salama pamoja na utunzaji wa mazingira, muwape
ushirikiano watakaporejea kufanya kazi,” alisema Ndugulile.
No comments:
Post a Comment