Mara nyingi tofauti nyingi sana hutokea
katika mahusiano yetu, ziko zile tofauti ndogo ndogo ambazo mara
nyingine hufukiwa na kutoongelewa, lakini ziko nyingine ambazo zaweza
kuanza kama cheche na baadae kuwa moto kubwa na kuelekea kuathiri
mahusiano yetu.
Tofauti hizi mara kwa mara zaweza kuwa na faida au
hasara katika mahusiano yetu. Zipo tofauti ambazo baada ya
kuzishuhulikia, wapenzi wemekuwa na mahusiano imara zaidi ya awali na
penzi lao limekuwa bora zaidi. Lakini zipo tofauti ambazo baada ya
kutokea tu, zimeua kabisa penzi na ukaribu uliokuwepo baina ya
wapendanao.
Wapo ambao hata tofauti kubwa ilipotokea na penzi baina yao
lilikufa na wakagawanyika. Athari zote hizi hutegemea na jinsi
wapendanao hao wanavyozitazama tofauti hizi na kuzishuhulikia. Wengine
wetu tumeshindwa katika mahusiano yetu kwa sababu tumeziangalia tofauti
zetu katika mtazamko hasi, na kwa hiyo kila tofauti kwetu tuniona ni
mbaya.
Katika makala hii nataka tusaidiane jinsi
ya kuzishuhulikia tofauti baina yetu, na tujue nini cha kufanya, na
nini sicho cha kufanya pale wapenzi au wanandoa wanapotofautiana.
Kama tayari mna vigezo hivi basi jaribuni
kuvizingatia kila mnapotofautiana, kwa mfano wapenzi wengi walio waelewa
wamejiwekea vigezo au masharti kwamba wakati wowote wa ugomvi au
kutofautiana lazima kila mmoja akumbuke kuwa kutofautiana hakumaanishi
kutokupendana. Wengine wamejiwekea kigezo kwamba, hata tofauti baina
yetu iwe kubwa vipi, kuachana kamwe haitakuwa upenyo au suluhisho. Kila
watu hawa wanapogombana akili zao zinakumbuka vigezo walivyojiwekea
wenyewe.
- Jitahidini kukaa mkiwa mmeangaliana (face to face seating)
Mnapo kaa mkiwa miili yenu imetazamana,
mnatoa nafasi kwa macho yenu pia kutazamana, na hii inawezesha kutuma
ujumbe kwamba wote mkotayari kusikilizana. Mmoja anapokwepesha macho
anaonyesha kutokuwa tayari kumsikiliza mwenzake na hivyo kufanya zoezi
la kutafuta suluhu kuwa gumu sana. Wapendanao wengine hushikana mikono
yote miwili, kama alama ya kuonyesha kujaliana ingawa wanapitia katika
fotauti nzito. Wakati mwenzako anatafuta jitihada za kukushika mikono
yako, jizuie usiseme maneno magumu au kuutupa mkono wa mwenzio, au
kuondoka kwa hasira pale ulipokuwa umeketi. Kama unalazimika kutaka
kuwapekeyako zaidi, tumia hekima kumwonyesha mwenzako kwamba una hitaji
faragha zaidi ili akuruhusu na kukuachia huru.
- Mawazo yenu na akili zenu zielekee tu katika malengo maalumu mliyonayo katika kutofautiana kwenu.
Maranyingi, katika kurushiana maneno,
matusi, kurushiana vitu na hata kupigana ni rahisi kutoka nje ya malengo
yenu. Jiulize, Je ni nini kilitufanya tutofautiane? Mfano: lengo
lenu lilikuwa kujaribu kutafuta muda wa kupunguza kazi za maofisini ili
walau mpate muda wenu binafsi. Au labda lengo lenu ni kujaribu
kuangalia uwezekano wa kuharakisha mchakato wa harusi yenu.
Mara mnapohama kwenye lengo lenu la awali
ni rahisi kuibua ugomvi mwingine na hivyo badala ya kuuzima moto
mkajikuta mnaupalia makaa. Kila wakati mnapoendelea na tafauti zenu,
mjiulize, je hiki ndicho kilichotufanya tutofautiane?
- Jaribu kuziandika au kuyaandika masuluhisho yote yanayowezekana
Najua ziko njia nyingi ambazo mtazichagua
za kuwasaidia kupunguza au kuondoa tofauti zenu nanjia hizo zaweza
kufeli. Ushauri ni kwamba, njia zote mnazoziona kuwa zinaweza kuwa na
msaada ziwekeni katika mtiririko maalumu.
- Mara
nyingi hatua hii hufanywa wakati lile fukuto la ugomvi limepoa, na kila
mmoja ameshaelewa sababu ya kutofautiana kwenu. Hapa sasa mzijadili
njia zote mnazoona zitakuwa suluhisho bila kujali ugumu au urahisi wa
utekelezaji wa njia hizo. Maoni mliyonayo katika utatuzi pia yawekeni
katika karatasi pembeni pasipo kuyafanyia tathmini yoyote.
- Jaribuni kuzitathmini njia zautatuzi mlizozipendekeza katika hatua ya nne
Baada ya kuziandika njia zote zinazoonekana
kuwa suluhisho la tofauti zenu, wote kwa pamoja muanze kuzitathimini
njia hizo mkiagalia madhara au matokeo ya kila mmoja.
Baada ya kuangalia madhara au matokeo
mtajikuta mmezipunguza njia hizo na kukuwachache sana, labda zaweza
kufikia mbili au tatu au hata moja na kwahivyo sasa mwaweza kuona ile
inayoweza kufanya kazi zaidi.
- Chagua njia au suluhisho lililokubaliwa na wote
Baada ya kujadili, kutathmini na kufikiri,
mwaweza kufikia uamuzi wa kuchagua njia moja ambayo wote mmeiafiki, au
ambayo mmoja amekubali kuiridhia. Kukua au kukomaa kwa akili na mapenzi
yenu kutaonekana katika uwezo wenu wa kufikia hatua hii ya sita. Mara
zote mmoja wenu asiwe wakuvutia upande wake tu. Lengo lisiwe kumtafuta
mshindi, kwa sababu, palipo na mshindi, pana mshindwa pia, na hakuna
anayependa kushindwa. Njia pekee ya suluhisho ni ile inayokaribia zaidi
na kulitatua tatizo na kuzikidhi haja za kila mmoja wenu.
- Tendea kazi muafaka au suluhisho mliloliamua
Ili kuepusha migogoro mingine tena, angalia
kila milichokiamua katika muafaka wenu, na vikumbuke vyote ili usije
kuvisahau na kurudia kosa. kumbuka makubaliano yenu, kuhusu nani
anatakiwa kufanya nini, wapi, lini, na vipi.
Kamwe usifanye yafuatayo mnapokuwa katika mgogoro baina yako na mpenzi wako:
- Kamwe msiitane majina yasiyorasmi wala msiyoyatumia kwa kawaida mfano; majina ya wanyama, vitu, majina ya kudharauliana na kushushiana hadhi.
- Kamwe msitishiane na kupigana mikwara kama vile vitisho vya talaka, kudhuru, au kujidhuru.
- Kamwe usiwaingize ndugu au wakwe kwenye mjadala usiowahusu au kuwachanganya ili kumuumiza moyo mwenzako.
- Kamwe msitukanane, kukosoana au kukejili maumbile ya mwenzako.
- Kamwe msitukanane, kukosoana au kukejeliana kuhusu uwezo wa akili au ufahamu wa mwenzako.
- Kamwe usimtilie shaka mpenziwako katika yale anayoyawaza au kuyaandika wakati huna uhakika.
- Kamwe kusiwepo na vurugu za kupigana baina yenu hata kama ni kwa vitisho tu.
- Kamwe usimuingilie mwenzako wakati anazungumza kitu, msikilize, subiri amalize na wewe useme.
- Kamwe usipayuke au kutumia sauti yako kubwa au kilio ili tu kutafuta ushindi.
- Kamwe kusiwepo na viapo visivyo na msingi wala kutupiana laana za maneno.
Daima jitahidi kufanya yafuatayo mnapokuwa katika migogoro
- Fanya kila linalowezekana kufikia muafaka kabla ya kumaliza mjadala au tofauti zenu. Kwamwe usiondoke, kusitisha au kutoroka katikakati ya mjadala au ugomvi wenu wakati haujaisha.
- Zungumza katika sauti ya kawaida pasipo kupayuka au kuhamaki.
- Kuwa na mtazamo chanya, usiingie katika ugomvi ukiwa na mtazamo wa kuvunjika kwa mahusiano.
- Tumia lugha inayokubaliwa pande zote mbili, matusi na kejeli havikubaliki.
- Weka mipaka ya ugomvi au tofauti zenu, jifunzeni kuzimiliki tofauti zenu na kuzifanya ziwe zenu binafsi. Mara nyingi sio hekima kila ugomvi wenu ujulikane na kila mtu kuanzia ndugu hadi wapitanjia. Epuka kuzozana mbele ya watoto.
- Jaribu kuwa muelewa na jitahidi kutilia maanani katika kusikiliza kile ambacho mwenzako anataka kukiwakilisha.
- Jaribu kukubali kukiri na kushuka badala ya kuwa mkwepa tuhuma ukitumia vijisababu vya kujilinda (defensive mechanisms)
- Jitahidi na penda kufikia muafaka na sio kutafuta kuwa mshindi katika tofauti mliyo nayo.
Credit:Chris Mauki
Asante kwa makala nzuri je kama mpenzi wako hataki kuongea na wewe utasuluhishaje hizo tofauti?
ReplyDelete