SERIKALI
imesema kwamba operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu katika Kanda ya Ziwa
itaanza kwa ghafla, huku ikiendelea kusisitiza kwamba watu
wanoaishi nchini bila taratibu za kisheria kuondoka kwa hiari na mali zao.
Kauli hiyo
imetolewa leo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi (pichani juu) wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wahamiaji haramu waliorejea kwao
baada ya agizo la Rais Jakaya Kiwete alilolitoa Juni 29, mwaka huu
katika ziara yake ya mkoa wa Kagera.
“Nimeshapewa
maelekezo rasmi na Rais Jakaya Kikwete ya kuwaondoa wahamiaji haramu
nitakapoona inafaa. Operesheni itaanza ghafla haiko mbali. Muda mwuafaka wa
kutekeleza vyombo vya dola vitasema.
“Tunatoa
wito waondoke wenyewe na mali zao bila kunyang’nywa. Wenye mali nyingi
wanatakiwa kutoa taarifa katika vituo vya polisi ili waweze kusindikizwa.
Hatutawavumilia wahamiaji haramu,” alisema Waziri Nchimbi.
Aliongeza
kuwa wahamiaji hao wanaotaka kuishi nchini wanatakiwa kurudi nchini kwao
kwanza na kufuata taratibu za kisheria kama ambavyo nchi nyingine zinavyofanya
mtu akitaka kuishi nchi yoyote anatakiwa kufuata taratibu hizo.
Waziri
alitoa onyo kwa viongozi wa vijiji wanaoshirikiana na wahamiaji hao kuwatunza
na kusema jambo hilo ni makosa kisheria , hivyo watakaobainika watachukuliwa
hatua za kisheria.
Akizungumzia
kuhusu takwimu za wahamiaji hao waliorejea nchini kwao mpaka sasa ni 10,672
kati ya hao Wanyarwanda ni 6,088, Warundi 4000 na Waganda 269
ambao wametoka mkoa wa Kagera. Kwa wa mkoa wa Kigoma ni Warundi
142, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nane na katika mkoa wa Geita
Wanyarwanda 126 na Warundi 39.
Hata
hivyo Waziri Nchimbi alisema kuna wahamiaji 14 wamerejea nchini
tena baada ya kurudi makwao na kuwataka wasilione jambo hilo kuwa ni mzaha.
Aidha
Waziri Nchimbi alisema Serikali ya Tanzania inashukuru ushirikiano unaotolewa
na nchi wanazotoka wahamiaji hao kwa kuwapokea vizuri.
Alifafanua
kuwa suala la kuwarudisha wahamiaji hao si la mara ya kwanza, lilishawahi
kutokea. Huku akisisitiza kwamba tatizo linatokana na sababu mipaka yetu
mikubwa na kuna watu wasio wazalendo ambao wanawapokea na
kuwakaribisha kwa kupatiwa zawadi. Hivyo Serikali inalifanyia kazi jambo hilo.
No comments:
Post a Comment