UPOKEAJI wa pingamizi za wagombea katika Uchaguzi Mkuu wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na TPL Board unatarajiwa kufungwa leo
mara baada ya pingamizi kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu TFF, Angetile
Osiah.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF, ilitangaza mchakato huo kuanzia Agosti 24
hadi leo saa 10:00 jioni kwa waweka pingamizi kuwasilisha pingamizi zao.
Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi huo, waweka pingamizi wote wanatakiwa
kuzingatia matakwa ya ibara ya 11(3) ya kanuni za uchaguzi katika
uwekaji pingamizi zao.
Mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Kamati ya Uchaguzi kesho
inatarajiwa kukutana na walioweka pamoja na waliowekewa pingamizi ili
kutoa utetezi wao juu ya pingamizi husika mbele ya kamati hiyo chini ya
Mwenyekiti wake Hamidu Mbwezeleni.
Baada ya kusikiliza pande hizo mbili, Kamati ya Uchaguzi itakuwa na
fursa ya kupitia pingamizi husika ili kuendelea kwa zoezi hilo.
Wakati Uchaguzi Mkuu wa TFF ukipangwa kufanyika Oktoba 27, ule wa Bodi ya Ligi utafanyika Oktoba 18, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment