SIMBA imerudia kauli yake kuwa Mrisho Ngassa anauzwa Sh150
milioni vinginevyo Yanga ihesabu maumivu, lakini akaongeza kuwa Shomari
Kapombe bei yake ni Sh480 milioni.

Hanspoppe alifafanua kuwa Ngassa alipojiunga na Simba kwa mkopo kutokea Azam, alisaini mkataba mwingine wa mwaka moja ambao utakwisha Mei mwakani. “Tena mkataba wenyewe tuliupeleka TFF tangu Desemba mwaka jana.
Sisi ambacho tunasema kama Yanga wanamtaka Ngassa walete pesa, bei yetu inafahamika ni Sh150 milioni,” alisema.
“Mimi ninachojua ni kwamba Ngassa anafundishwa kuzungumza na baadhi ya watu wa Yanga, lakini anajua ukweli na kwa sababu ameonyesha kuwa anataka kuchezea Yanga sisi hatuna tatizo, walete hizo Sh150 milioni,” alisema.
Ngassa amekuwa akirudia mara kwa mara kuwa hajasaini Simba na kwamba mkataba anaoutambua ni ule ambao amesaini Yanga. Msimu uliopita, Simba ilidai pia kuwasainisha Kelvin Yondani na Mbuyu Twite, lakini wote wakaishia Yanga.
Katika hatua nyingine, Hanspoppe alisema kiraka wao, Kapombe ambaye amekuwa akijaribiwa na timu mbalimbali Uholanzi na Ufaransa watamuuza kwa Dola 300,000 (Sh480 milioni).
“Kuna timu ya Cannes ya Ufaransa wameridhika na mchezaji huyo, lakini sisi bei yetu ni hiyo yaani Dola 300,000 (Sh480 milioni),” alisema Hanspoppe.
Wakati huohuo, Hanspoppe amesema karibu klabu tatu zilizokuwa zinamtaka Amri Kiemba zimesitisha mpango huo kwa sababu ya umri wa Kiemba. “Kila wanapoomba CV, tukiwapelekea wanaona umri wake mkubwa, wanasitisha mpango wao,” alisema Hanspoppe. Kwa mujibu wa hati ya kusafiria, Kiemba ana umri wa miaka 31.
CHANZO CHA HABARI NI MWANASPORTS.
No comments:
Post a Comment