KLABU ya Yanga imepanga kumalizana na nyota wake wa zamani,
Stephano Mwasyika na Shadrack Nsajigwa, wanaoidai sh mil. 16, ikiwa ni
siku chache tangu wafikishe madai yao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
kuomba msaada wa kupata haki yao.
Habari zilizotufikia siku jana na kuthibitishwa na kiongozi
mmoja ambaye hata hivyo hakutaka jina lake litajwe kwa sababu maalumu,
Yanga isingependa kuingia kwenye mvutano na nyota hao, hivyo imepanga
kumaliza suala hilo wiki ijayo.
Mbali ya Nsajigwa na Mwasyika pia chanzo hicho kimedokeza kuwa Yanga
itatoa kiasi cha shilingi mil. 100 kwa wachezaji kwa kutwaa ubingwa wa
Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita uliofikia tamati Mei 18, ikiwa ni
utekelezaji wa ahadi kwao.
Chanzo hicho kilisema uongozi wa klabu hiyo unasikitishwa na madeni
mengi waliyoyakuta wakati wanaingia madarakani Julai 15, mwaka jana,
wamekuwa wakijitahidi kuyalipa kulinda hadhi ya klabu hiyo.
“Tumesikia juu ya kina Mwasyika na Nsajigwa, sisi kama viongozi wapya,
kiukweli tumeumia sana hasa ukiangalia mchango wao kwa Yanga, ni kweli
wanatudai, sisi tunahangaika kuyalipa madeni ambayo ni mengi,” alisema
kiongozi huyo.
Alisema mbali ya wachezaji hao, wapo wengine ambao wamekuwa wakiwadai,
hivyo wako mbioni kumaliza madeni hayo kwa lengo la kufanya kazi kwa
ufanisi kama walivyotumwa na wapiga kura wao na kuongeza kuchelewa
kulipwa ni suala la kawaida.
“Hata wewe kuna siku bosi wako anachelewa kukulipa, ila kuna njia za
kuzungumza naye na ukiona amekwambia subiri kidogo, ujue anatafuta mbinu
ya kumalizana nawe, na sisi tunajua wajibu wetu, hatuwezi kuwazima, ni
haki yao,” alisisitiza.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Lawrence Mwalusako, alisema
mpango wao ni kuwalipa wachezaji hao kwani ni kweli wanaidai klabu hiyo
fedha ambazo ni haki yao kuzipata kutokana na jasho lao.
No comments:
Post a Comment