MATUKIO ya ujambazi katika Jiji la Dar es Salaam yamezidi
kushika kasi baada ya jana majira ya saa 3:00 asubuhi watu wawili
waliokuwa katika pikipiki aina ya Boxer kumpora mwanamke mamilioni ya
fedha kwa kutumia silaha.
Tukio hilo limetokea siku mbili baada ya matukio mawili ya aina hiyo
kutokea katika jiji hilo mojawapo likitokea katika Benki ya Habib,
iliyopo makutano ya Barabara ya Livingstone na Uhuru na kufanikisha
uporaji wa mamilioni ya shilingi za Kitanzania pamoja na dola za
Marekani 181,885.
Jingine lilitokea maeneo ya Gymkhana, makutano ya Barabara ya Barack
Obama na kuhusisha raia wawili wa Kenya ambao ni ndugu, Mark Rubila(16)
na Sila Rubila(21) kutoka mji wa Kakamega ambao walimuua kikatili dereva
teksi Ramadhani Mahembe(38), maarufu kama ‘Mjomba Mjomba’ au ‘Papaa’
mkazi wa Buguruni Chama.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio la jana, mwanamke huyo aliporwa fedha
hizo katika kituo cha basi cha Kwa Aziz Ally, Wilaya ya Temeke, dakika
chache baada ya kushuka ndani ya daladala akitokea Mbagala.
“Baada ya kushuka mwanamke huyo ambaye alikuwa na begi alisimama
kituoni hapo akisubiri usafiri mwingine lakini ghafla ilikuja pikipiki
aina ya Boxer iliyokuwa na watu wawili na kumpora begi hilo lililokuwa
na pesa ambazo kiasi chake bado hakijajulikana,” alisema shuhuda mmoja.
Kabla ya kupora, majambazi hayo walifyatua risasi ambayo ilimjeruhi
mwanamke huyo na abiria mwingine aliyekuwa kituoni hapo akisubiri gari.
“Hili tukio ni la kupanga kwani haiwezekani mtu atokee sehemu akiwa na
mzigo wake kisha afikie kuporwa hivi hivi, inaonekana kuna watu walijua
kila kitu kuhusu mwanamke huyo na kumfuatilia na walijua fedha hizo
anazipeleka wapi,” alisema shuhuda mwingine.
Katika hatua nyingine, watuhumiwa waliohusika katika tukio la mauaji
ya dereva teksi Mahembe, walitoa siri kuwa walitaka kupora gari la
dereva huyo ili wakaliuze.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
alisema polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wengine maeneo ya
Kimara Bonyokwa wakiwemo raia wa Kenya, wakiwa na gari aina ya Toyota
Corolla lenye namba za usajili T 230 ABV ambalo pia ni la wizi.
Watuhumiwa hao ni Ramadhani Rashidi(32) na Hamisi Rashidi(36).
No comments:
Post a Comment