Habari na Happiness Katabazi wa Tanzania Daima.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imewahukumu
kwenda jela miaka tofauti washitakiwa watatu waliokuwa wakikabiliwa na
kesi ya wizi wa sh bilioni 1.1 katika akaunti ya madeni ya nje (EPA)
katika Benki Kuu ya Tanzania.
Hatua hiyo ni baada ya kuwakuta na hatia katika makosa mbalimbali,
likiwemo la kughushi hati ya kuhamisha deni toka Kampuni ya Marubeni ya
Japan kwenda Kampuni ya Changanyikeni Residential Complex ya nchini.
Hukumu hiyo ya kesi ya jinai iliyokuwa ikiwakabili Bahati Mahenge,
Manase Makalle, Davis Kamungu, Geofrey Mosha na Edda Mwakale ambaye ni
mke wa mshitakiwa wa pili, ilitolewa na jopo lililokuwa likiongozwa na
Jaji Sekela Mushi, Jaji Sam Rumanyika na
Hakimu Mkazi Lameck Mlacha
ambaye aliisoma kwa niaba ya wenzake.
Mlacha alisoma hukumu hiyo kwa kuanza kuikumbusha mahakama kuwa hati
ya mashitaka ilikuwa na mashitaka tisa na kwamba kosa la kwanza ni kula
njama kinyume na kifungu cha 384 cha sheria ya kanuni ya adhabu ya
mwaka 2002.
Alisema kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo kati ya Desemba 23
mwaka 2003 na Oktoba 26 mwaka 2005, ambapo kwa pamoja na watu wengine
ambao hawapo mahakamani walitenda kosa hilo na kuiibia BoT.
Hakimu Mlacha alisema baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vyote,
mahakama yake inawatia hatiani Mahenge na Manase na kuwahukumu kwenda
jela miaka mitano huku akiwaachia huru washitakiwa wengine.
Katika kosa la pili la kuwasilisha nyaraka za kutaka kampuni yao ya
Changanyikeni isajiliwe na Brela huku wakionyesha jina la kufikirika la
Samson Mapunda kuwa ndiye mkurugenzi wa kampuni hiyo, hakimu Mlacha
pia alisema Mahenge na Manase walitenda kosa hilo na hivyo mahakama
yake inawahukumu kwenda jela miaka mitano.
Kosa la tatu lilikuwa likimkabili Mahenge pekee akidaiwa kutoa
nyaraka za uongo za kuomba usajili wa kampuni zikionyesha Mapunda ndiye
mkurugenzi wa Changanyikeni, na hivyo kuwezesha kampuni hiyo kupewa
usajili na Brela. Mahakama ilimtia hatiani na kumfunga miaka saba
gerezani.
Hakimu Mlacha alilitaja kosa la nne kuwa la Kampuni ya Changanyikeni
Residential Complex, ambalo washitakiwa wamejipatia usajili toka Brela
kwa nia ya udanganyifu kwa kutumia jina la kufikirika ambapo mahakama
iliwatia hatiani tena Mahenge na Manase kwa kuwahukumu kifungo cha
mwaka mmoja jela.
Katika kosa la tano la kughushi ambalo linawakabili washitakiwa wote,
hakimu alisema katika maelezo ya onyo alilowapa wachunguzi wa kesi
hiyo, Mahenge alikiri kuwa yeye alikuwa akitumwa kuchukua hundi za
malipo ya kampuni hizo mbali na kwamba ndiye aliyekwenda kupeleka fomu
Brela za kusajili kampuni yao ya Changanyikeni.
Alisema kuwa Mahenge alikuwa akisaidiana kufanya kazi hiyo na
mshitakiwa Manase, hivyo mahakama hiyo imewatia hatiani Mahenge na
Manase na Edda ambao ni mke na mume na kwamba watakwenda jela miezi 18.
Kosa la sita liliwakabili washitakiwa wote ambalo ni la kughushi hati
ya kuhamisha deni lililokuwa likionyesha Kampuni ya Marubeni ya Japan
imeridhia Kampuni ya Changanyikeni idai deni lake jambo ambalo si
kweli.
“Licha upande wa utetezi kudai hati hiyo ya kuhamisha deni ilikuwa ni
halisi, lakini sisi kama mahakama tulipata wasaa tukaikagua kwa
makini, tukabaini hata hiyo kampuni ya Marubeni haikutia saini katika
hati hiyo, na kampuni ya Changanyikeni ilisaini hati hiyo bila kuwepo
shahidi wa kushuhudia tukio hilo.
“Hati hiyo inaonyesha ilisainiwa katika mgahawa wa City Garden Dar es
Salaam, na tulijiuliza Marubeni ni kampuni kubwa kwanini haikutia
saini katika hati hiyo, na mwisho wake mahakama hii ikakubaliana na
upande wa jamhuri kuwa hati hiyo ilikuwa imeghushiwa,” alisema.
Alisema kuwa kwa kosa hilo, mahakama inawatia hatiani Mahenge na Manase na hivyo wataenda jela miezi 18.
Shitaka la saba liliwakabili washitakiwa wote ambalo ni la
kuwasilisha hati hiyo ya kuhamisha deni iliyoghushiwa na kwamba
mahakama yake imemtia hatiani Mahenge ambaye atakwenda jela mwaka
mmoja.
Kuhusu shitaka la nane ambalo ni wizi na shitaka la tisa lilikuwa ni
la kujipatia kiasi hicho cha fedha toka BoT, hakimu Mlacha alisema
mahakama yake inawaachilia huru katika makosa hayo mawili.
Hata hivyo hakimu Mlacha alisema ushahidi ulioletwa na upande wa
jamhuri umeshindwa kuishawishi mahakama imuone mshitakiwa wa tatu
(Davis Kamungu) na wanne (Geofrey Mosha) wana hatia katika kesi hiyo na
kwa sababu hiyo ikawaachilia huru.
Baada ya hakimu Mlacha kuwatia hatiani washitakiwa hao, wakili
Mwanadamizi wa serikali Shadrack Kimaro alidai upande wa jamhuri hauna
rekodi za uhalifu za washitakiwa waliotiwa hatiani ila wanaiomba itoe
adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
Aliomba mahakama itumie kifungu 384(1) na 358(1) cha Sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, kuwaamuru washitakiwa
waliotiwa hatiani kurejesha kiasi hicho cha fedha serikalini.
Kwa upande wake wakili wa washitakiwa, Tarimo, aliomba mahakama
iwapatie adhabu ndogo kwani hii ni mara yao ya kwanza kukutwa na hatia,
na kwamba Manase na Edda ni mke na mume wana familia inawategemea na
kudai kuwa Edda anasumbuliwa na maradhi ya uzazi hivyo anaomba wapewe
adhabu ndogo.
Hakimu Mlacha alisema amesikiliza maombi ya pande zote mbili na
kwamba mahakama hiyo inaamuru Mahenge na Manase warejeshe kiasi hicho
cha fedha na kwamba adhabu hiyo itakwenda pamoja.
Kwa maana hiyo Mahenge peke yake atakwenda jela miaka saba, Manase mitano na Edda miezi 18.
Baada ya hukumu hiyo kumalizika kusomwa baadhi ya ndugu na jamaa wa
washitakiwa hao waliangusha vilio mahakamani hapo na wanausalama
waliwachukua wafungwa hao na kuwapeleka gerezani.
Novemba 2008, Wakili Kiongozi wa Serikali Stanslaus Boniface ambaye
sasa ni marehemu alidai washitakiwa hao walitenda makosa hayo.
Hii ni kesi ya tano sasa ya EPA kati ya kesi 12 zilizofunguliwa
mahakamani hapo Novemba 2008 na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk.
Eliezer Feleshi kufuatia kumalizika kwa uchunguzi wa Tume ya Rais
Jakaya Kikwete ya kuchunguza wizi huo.
No comments:
Post a Comment