SACP mstaafu James Kombe enzi za uhai wake.
Aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani
Nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (Mstaafu) James Kombe amefariki
dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Ocean Road jijini
Dar es Salaam.
Akizungumzia kifo hicho Msemaji wa Jeshi la Polisi
Nchini, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Advera Senso alisema, Kombe
alifariki Oktoba 22 mwaka huu na taratibu za mazishi zinaendelea
nyumbani kwa mtoto wake, Mtoni Kijichi, Dar es Salaam.
Aidha habari
tulizozipata kutoka ndani ya jeshi la polisi zinasema marehemu
atasafirishwa na kupelekwa Moshi kwa mazishi kesho Oktoba 23.
Akizungumzia historia yake, Kamanda Senso alisema marehemu Kombe
alizaliwa mwaka 1950 huko Mwika mkoani Kilimanjaro na alijiunga na jeshi
la polisi Machi 15, 1970 baada ya kuhitimu elimu ya sekondari mwaka
1969 nchini Uganda.
Akiwa mtumishi wa jeshi hilo Kombe alipandishwa vyeo na kupewa madaraka mbalimbali.
Baadhi ya vyeo alivyopitia na miaka ya kupata vyeo hivyo katika
mabano ni pamoja na Sagenti wa Polisi (1973), Mkaguzi Msaidizi wa Polisi
(1977), Mkaguzi wa Polisi (1984), Mrakibu Msaidizi (1986), Mrakibu wa
Polisi(1991), Mrakibu Mwandamizi (1995), Kamishna Msaidizi wa Polisi
(1998) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (2002) hadi alipostaafu
mwaka 2010.
Baadhi ya nafasi alizowahi kuzitumikia katika Jeshi la
Polisi ni pamoja na kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) katika wilaya za
Dodoma, Tarime, Serengeti na Arusha pamoja na kuwa Mkuu wa Polisi wa
Mkoa (RPC) katika mikoa ya Lindi, Arusha, Kigoma pamoja na Mkuu wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia Tanzania (FFU) na hadi anastaafu alikuwa Mkuu
wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania.
No comments:
Post a Comment