GUMZO kubwa kwa sasa ni mechi ya Ligi Kuu kati ya watani wa
jadi, Simba na Yanga itakayochezwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Esrael Nkongo, inapigwa baada
ya siku 52 tangu watani hao wakutane mara ya mwisho Mei 18, ambapo Yanga
walishinda mabao 2-0 chini ya Kocha Ernie Brandts.
Mabao hayo ambayo yalipeleka faraja Jangwani katika mechi hiyo ya
kufunga msimu wa 2012/13, yalifungwa na Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza.
Kipigo hicho kinaifanya Simba chini ya Kocha Abdallah ‘King’ Kibadeni
kuwa na deni, huku Yanga wakitaka kushinda kuendeleza ubabe mbele ya
mtani wake.
Licha ya Yanga kushinda 2-0, bado inatamani kulipa kisasi cha mabao
5-0 cha Mei 6, 2012, hivyo mechi ya leo kuwa yenye ushindani mkubwa
zaidi kwa kila moja kupigania ushindi.
Timu hizi zinakutana huku Simba ikiwa ya tatu kwenye msimamo wa ligi
kwa pointi 18, nyuma ya Azam na Mbeya City zenye pointi 20 kila moja, na
Yanga nafasi ya tano ikiwa na pointi 15.
Wakati Simba ikiwa na hesabu za kurejea kwenye usukani kwenye msimamo
wa ligi hiyo iliyoingia raundi ya nane tangu ilipoanza Agosti 24, Yanga
watakuwa wakitaka kufuta pengo la pointi tatu baina yao.
Akizungumzia mechi hiyo kutoka kisiwani Pemba, kocha msaidizi Fred
Felix Minziro alisema ukiondoa Salum Telela ambaye yu majeruhi, wengine
wote wapo fiti. Msafara wa timu hiyo ulitarajiwa kutua jijini Dar es
Salaam jana usiku au alfajiri ya leo.
Minziro alisema kwa mazoezi waliyofanya kabla na wakati wakiwa kambini
Pemba, hawana shaka ya ushindi kwani wachezaji wamekuwa kwenye ari
kubwa, japo hapendi kusema mengi, zaidi ya kuwataka wapenzi na mashabiki
wa timu hiyo kufika kwa wingi Uwanja wa Taifa.
“Tumejiandaa vizuri kwa mechi, wachezaji wote wapo fiti ukimuondoa
Telela. Sitaki kusema mengi. Wapenzi na mashabiki wa soka waje uwanjani
wajionee burudani,” alisema.
Alisema mbali ya maandalizi yao kwenda vizuri kwa maana ya programu
yao iliyowapeleka Pemba, pia wamepata baraka za wazee wa huko ambao
wamewatakia kila la heri kuelekea mechi hiyo kwa kuwaombea dua.
“Wazee wa Pemba wametupokea vizuri, tuko nao bega kwa bega.
Wamewaombea wachezaji dua ya kuwatakia ushindi, hivyo tunaamini mambo
yatakwenda vizuri japo mpira ni dakika 90,” alisema Minziro.
Kwa upande wa Simba, Kocha msaidizi Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema
vijana wao wapo vizuri kuwakabili Yanga leo kwani kila mmoja yu fiti
akisubiri kwa shauku kubwa kupangwa katika mpambano huo wa kukata na
shoka.
Julio alisema wachezaji wapo vizuri kuelekea mechi ya leo, licha ya
fitna dhidi yao ikiwemo madai ya benchi la ufundi kuwabagua wachezaji
katika upangaji wa kikosi, akisema ni mbinu chafu za kutaka kuwavuruga.
Viingilio vya mechi hiyo, ni sh 30,000 kwa viti vya VIP A; VIP B sh
20,000; sh 15,000 kwa viti vya VIP C; sh 10,000 kwa viti vya rangi ya
chungwa; Bluu sh 7,000 na Kijani sh 5,000.
No comments:
Post a Comment