MTANGAZAJI wa kituo cha runinga cha ITV, Ufoo Saro amenusurika
kifo baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi mbili tumboni na
kifuani na mzazi mwenzake, Antel Mushi ambaye ni mhandisi wa mawasiliano
kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa (UN) kinachofanya kazi nchini Sudan.
Katika tukio hilo la kutisha lililotokea jana saa 12:30 asubuhi, Mushi
pia alimuua mama mzazi wa Ufoo kwa kumpiga risasi kifuani na kisha
kujiua mwenyewe kwa kujipiga risasi eneo la kidevu, iliyomfumua
kichwani.
Mauaji hayo yalitokea eneo la Kibamba, Njia panda ya Shule, nyumbani
kwa mama mzazi wa mtangazaji huyo, Anastazia Salo (58) ambako wawili
hao; Ufoo na mpenzi wake walikuwa wamefika muda mfupi kabla tukio.
Mushi na Ufoo wamezaa mtoto mmoja, Alvinen Mushi (10), na wakati
wanatoka nyumbani kuelekea kwa mama mzazi wa mtangazaji huyo, walimuacha
mtoto wao akiwa amelala na dada yake wa kazi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius
Wambura, tukio hilo linahusishwa na ugomvi wa kifamilia ambao hadi sasa
haujafahamika chanzo chake.
Shuhuda wa tukio hilo, Habelis Innocent ambaye ni ndugu wa karibu wa
Ufoo, aliliambia gazeti hili kuwa mtangazaji huyo alijeruhiwa vibaya
eneo la tumboni na mkononi.
Habelis alisema kuwa mapema alfajiri jana, Ufoo na Mushi waliondoka
nyumbani kwao eneo la Magari Saba kuelekea Kibamba kwa mama wa Ufoo,
kwamba wakiwa njiani mtangazaji huyo alimpigia mama yake simu na
kumwambia aondoke nyumbani haraka.
Alisema kuwa Ufoo alimtaka mama yake kuondoka nyumbani kwa kuwa
mchumba wake ana hasira, na hivyo anaweza kufanya fujo, lakini baada ya
mama huyo kupata taarifa hizo hakuweza kuondoka haraka hadi walipofika.
Habelis alifafanua kuwa walipofika nyumbani hapo waligonga mlango na
kisha mama yao kuwafungulia. Kwamba muda huo alikuwa anajiandaa kwenda
kanisani, lakini hakuweza tena kuendelea na alichokua anakifanya, badala
yake aliketi kuwasikiliza kilichowaleta.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, wakati mama, Ufoo na Mushi wakiwa sebuleni
yeye alikuwa chumbani huku akisikia mazungumzo yaliyodhihirisha
kulikuwa na mgongano ambao ulitakiwa kutafutiwa ufumbuzi.
Alisema kuwa wakati mazungumzo hayo yakiendelea, ghafla akasikia mlio
wa risasi na sauti ya mama akiomba msaada kutoka kwake, akimtaka atoke
haraka aliko ili kama kufa wafe wote.
Habelis alisema kuwa alipotoka alikuta tayari mama yake ameuawa na baadaye Mushi alimpiga risasi ya tumboni na mkononi Ufoo.
“Baada ya kushuhudia tukio hilo, nilianza kujihami na kukimbilia
kwenye chumba kingine huku nikiwaambia wenzangu niliokuwa nimelala nao
wasitoke nje.
“Wakati natafuta namna ya kujihami kwa kupanda darini, Mushi alipiga
risasi nne mfululizo ili mlango ufunguke zinipate, lakini alishindwa na
hivyo alihamia chumba alichokuwa mdogo wa Ufoo na kupiga risasi mbili
mfululizo ili zimpate yoyote aliyekuwemo,” alisema.
Aliongeza kuwa wakati akipiga risasi hizo, vijana waliokuwa katika
chumba hicho walifanya jitihada za kubomoa dari na kisha kupata upenyo
wa kujificha darini na hatimaye Mushi akawakosa.
Aliwataja wenzake hao waliokoswakoswa na risasi katika tukio hilo kuwa
ni Godluck Saro na Jonasi Saro na kuongeza kuwa baadaye Mushi
alikimbilia jikoni na kukuta jiko la gesi, aliwasha na kuchoma nguo ili
nyumba ilipuke waliomo ndani wateketee.
Shuhuda huyo alisema kuwa baada ya kuchoma nguo, Mushi alirudi
sebuleni na kisha kujimalizia mwenyewe kwa kujipiga risasi na kupoteza
maisha papo hapo.
Ufoo alikimbizwa Hospitali ya Tumbi, Kibaha ambako alipatiwa huduma ya kwanza na kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Kamishna Suleiman Kova, uchunguzi wa awali uliofanyika katika gari
alilotumia Mushi walikuta begi likiwa na kompyuta ndogo (laptop), kamba
za kujinyongea, panga, pingu, kisu na risasi.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini Muhimbili, Kova alisema
kwa mujibu wa madaktari, hali ya mgonjwa ilikuwa inaendelea vizuri na
alikuwa akitarajiwa kufanyiwa upasuaji nyakati za mchana.
Kova alisema japo mhusika alijiua baada ya kumuua mkwewe na kumjeruhi
kwa risasi Ufoo, bado kitendo hicho hakiliondolei jeshi hilo kuchunguza
tukio hilo.
Alisema kuwa wanatarajia Ufoo atakuwa miongoni mwa watu watakaolisaidia jeshi hilo kupata taarifa zaidi za tukio hilo.
Naye, ofisa upelelezi wa makosa ya jinai, Ahmed Msangi alisema hadi
sasa hakuna taarifa kamili, bali jeshi limejigawa sehemu tatu, kila
kundi likikusanya taarifa.
Alisema baada ya makundi hayo ambayo yalikuwa katika maeneo ya
nyumbani lilikotokea tukio, Tumbi hospitali na Muhimbili, kukusanya
taarifa watazitoa kwa waandishi wa habari.
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi alisema
kipindi hicho madaktari walikuwa wakiendelea na uchunguzi kwa ajili ya
kukamilisha upasuaji.
Alisema kuwa hali yake Ufoo sio mbaya bali ilikuwa inaendelea vizuri akiwa chini ya uangalizi wa madaktari.Credit tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment