*Tamasha lile lile, muonekano tofauti
* Kumwaga magari sita, Pikipiki 14, Simu 200, na zagazaga kibao!
Mtiti
wa kuelekea tamasha kubwa na zuri la burudani la kila mwaka
linaloratibiwa na Clouds Media group, maarufu kwa jina la Fiesta
unatarajiwa kutimka kuanzia Jumapili ijayo katika viwanja vya TIA jijini
Mbeya ambapo Bonanza la mashabiki wa timu za Ulaya watamenyana katika
kinyang'anyiro cha Fiesta Soccer Bonanza, ikiwa ni sehemu tu ya
shamrashamra ya tamasha hilo kwa mwaka huu.
Michezo hii
itaendelea kwa mikoa kadhaa ikiwa ni sehemu tu ya shamra shamra hizo
lakini pia kutakuwa na matamasha madogo madogo kama kumsaka MC Shujaa,
kusaka kundi bora la kucheza muziki, shindano ambalo limepachikwa jina
la Dance la Fiesta, na Fiesta Supa Nyota ambayo itamtoa mwimbaji mkali
kabisa ambaye hajawahi kuonekana kwenye tasnia hii ambayo yatafuatiwa na
ziara ya mikoa 14, kusherehekea mwaka mwingine wa mafanikio ya
kiburudani kwa amani huku mashabiki wa muziki wa kizazi kipya
wakiburudika na kujumuika kwa pamoja.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Clouds Media Group, Joseph Kussaga ameiambia Mwananchi Starehe kwamba
hili ni Tamasha la 11 tangu kuanzishwa kwake, na ni tamasha ambalo
limesaidia kwa kiasi kikubwa kuleta hamasa kwa mashabiki wa muziki ambao
kwa siku za nyuma ilikuwa ngumu kwao kukutana uso kwa uso na msanii
wanayempenda.
"Fiesta ndiyo mwanzilishi wa mkutano wa uhakika wa
uso kwa uso kati ya shabiki na msanii ambapo hapo awali ilikuwa ni mpaka
msanii aalikwe, au afikirie mwenyewe kwenda lakini Fiesta ni uhakika wa
msanii anayevuma kukutana na shabiki wake kwa wakati muafaka".
Kussaga
aliitamka rasmi kauli mbiu ya tamasha hilo mwaka huu kuwa burudani
itakuwa ile ile lakini muonekano ndio utakuwa tofauti kwani jukwaa
litakuwa sio lile ambalo watu wamelizoea na pia kutakuwa na vyombo vya
muziki ambavyo vitamsababishia shabiki wa muziki kupata muziki mzuri
masikioni mwake usiokuwa na bugudha, ambao pia ataufurahia.
Tamasha
la mwaka huu pia linatarajia kuwazawadia mashabiki wake magari sita
yenye thamani ya shilingi milioni nane kila moja, aina ya Toyota Vitz,
Pikipiki aina ya Boda boda takriban kumi na nne huku kila moja ikiwa na
thamani ya shilingi Milioni moja na nusu, Simu 200, huku hamsini kati ya
hizo ziliwa ni Blackberry zenye thamani ya shilingi laki saba kila moja
na zilizobaki zikiwa ni Nokia dabo dabo zenye thamani ya Tshs 80,000.
Kuhusu
wasanii watakaoshiriki kwenye tamasha hili, Kussaga ameiambia Starehe
kwamba kutakuwa na wasanii wachanga ambao hawajawahi kuonekana katika
jukwaa, na pia kutakuwa na wasanii wakubwa kabisa ambao kwa pamoja
wataunganisha nguvu na kuleta kitu kikubwa na kizuri kwenye tasnia ya
burudani ambacho mwisho wa siku kila mmoja wa mashabiki wa muziki wa
kizazi kipya atafurahia.
Shughuli nzito inaanza Julai, ambapo
shughuli mbali mbali zitakuwa zikifanywa kwa kwezi mzima na baada ya
hapo sasa mwezi wa nane ndio kitu kizima cha Fiesta yenyewe kitaanza.
Shughuli
ya dace la Fiesta itafanyika katika mikoa ya Arusha Jumamosi hii,
katika Club ya Mawingu, na kisha wiki zinazofuata itahamia kwenye mikoa
ya Mwanza katika Club ya lips tarehe 7 Julai, kisha La Cassa Chica Tanga
tarehe 14 Julai na kisha Maisha Club, Dar es Salaam, itakuwa ni Julai
17.
Mpaka sasa, shughuli ya Soccer Bonanza imeidhinishwa kwa mikoa minne tu ambayo ni Mbeya, mwanza Moshi na dar es Salaam.
Kuhusiana
na Mc Shujaa, mpaka sasa ni dar, mwanza na Arusha ndio kunaonekana
kwenye ratiba, lakini kadri muda unavyozidi kuendelea uongozi umeahidi
kutoa ratiba endelevu.
Mikoa ambayo Fiesta itapita kwa mwaka huu
imeidhinishwa kuwa ni Moshi, Arusha, Musoma, Shinyanga, Mwanza,
Morogoro, Dodoma, iringa, Mbeya Singida, Tabora, Tanga, Zanzibar, na
kisha Dar es salaam
No comments:
Post a Comment