JESHI la Polisi mkoani Singida, linamshikilia mwanamke, Maria
Chibago (33), mkazi wa Kijiji cha Mpapa, Tarafa ya Nkonko wilayani
Manyoni kwa tuhuma za kupatikana na vipande saba vya meno ya tembo,
kinyume cha sheria.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela alisema tukio hilo
limetokea juzi, majira ya saa 11:00 jioni katika Kijiji cha Mpapa.
Kwa mujibu wa Kamwela, mtuhumiwa alikuwa ameyahifadhiwa meno hayo
kwenye mfuko wa sandarusi na kufukiwa ardhini katika eneo la nyumbani
kwake.
Alisema upatikanaji wa nyara hizo, ulifanikiwa kutokana na taarifa za
siri kutoka kwa raia wema, kwamba familia ya Maria hujihusisha na
shughuli za ujangili, akiwemo mumewe.
Kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, mume wa Maria, Tadei Msagala pamoja na
washirika wake, baada ya kushitukia mtego wa polisi, walifanikiwa
kukimbia.
Katika hatua nyingine, Kamanda Kamwela alisema wanamshikilia Hamisi
Seleman (30) mkazi wa Kijiji cha Nsemembo, Wilaya ya Manyoni kwa tuhuma
ya kumiliki bunduki aina ya rifle na risasi nne.
“Mtuhumiwa Hamisi amekamatwa Septemba 27, mwaka huu saa 11.00 jioni
akiwa ameificha silaha hiyo nzito kwenye mfuko wa sandarusi na kuifunga
kwenye baiskeli yake akielekea kwenye uwindaji haramu,” alisema.
No comments:
Post a Comment