Habari na Tanzania Daima.
ASKARI wa Kituo cha Polisi Mangaka, Wilaya ya Masasi, mkoani
Mtwara wanadaiwa kumuua kwa kipigo mkazi wa Kata ya Mbonde, Abbas
Maagano.
Habari zilizoifikia Tanzania Daima Jumapili, na kuthibitishwa na kaka
wa marehemu, Bedda Faustine, zilidai tukio hilo lilitokea Oktoba 10,
mwaka huu.
Faustine alisema kuwa mdogo wake alifuatwa na askari polisi, wanajeshi
pamoja na askari wa maliasili nyumbani kwake siku ya Alhamisi iliyopita
wakiwa kwenye magari mawili na kufanya ukaguzi wakidai ana silaha.
“Walisema ndugu yetu anamiliki silaha kinyume na sheria pamoja na
kufanya vitendo vya kijangiri jambo ambalo tulilikana, kwakuwa hahusiki,
kwani alikuwa ni mjasiriamali wa kawaida aliyekuwa akimiliki duka la
kuuza bidhaa mbalimbali mjini hapa,” alisema Faustine.
Alisema kuwa baada ya ukaguzi kufanyika bila kupata walichokitarajia,
walimchukua ndugu yao kwenda kituo cha Mangaka akiwa na wenzake watano.
Faustine alisema kuwa baadae wale wenzake watano, waliachiwa na kukiri
kuwa walipigwa sana walipokuwa kituoni, lakini mdogo wake alizuiliwa.
“Baada ya wale wengine kuruhusiwa ndipo sisi tulipopata taarifa ya
kwamba mdogo wangu amefariki, tukaamua kwenda kituoni kupata uhakika
kutoka kwa mkuu wa kituo ambaye alitupeleka hospitali ambako daktari
alithibitisha ni kweli Abbas amefariki,” alisema Faustine.
Aliongeza kuwa baada ya kupewa taarifa hizo walitaka kujua ni nini
kilichomuua ndugu yao ilhali wakati akikamatwa alikuwa na afya njema.
Alibainisha kuwa daktari aliwaambia kuwa hali ya ndugu yao ilibadilika
ghafla alipokuwa kituo cha polisi na hivyo kusababisha kifo chake.
Faustine alisema walipotaka kuuona mwili wa marehemu, polisi walikuwa
wakiwazungusha ingawa baadae walifanikiwa kuuona ambapo walibaini una
majeraha makubwa yaliyotokana na kipigo.
“Tulipombana sana daktari aliyejulikana kwa jina la Kumwembe ambaye
ndiye aliyetoa ripoti ya kifo cha Abbas, alikiri ni kweli ndugu yetu
alifariki kutokana na kipigo,” alisema.
Faustine alisema kuwa pamoja na daktari huyo kuwafichulia ukweli,
lakini alikataa kuwapa karatasi zenye ripoti ya marehemu kwa kuhofia
usalama wake hadi walipoomba wapewe mwili huo kwa ajili ya kwenda kuzika
kwa kuwa ulishaanza kuharibika na kutoa harufu.
Marehemu alizikwa jana kijijini kwake Mbonde huko Masasi.
Tanzania Daima Jumapili, iliwasiliana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya
Nanyumbu, aliyetambulika kwa jina la Joshua Mafurango ambaye alisema si
msemaji.
Mafurango alilitaka gazeti hili kuwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Mtwara, Zalothe Stephen ambaye hata hivyo hakuweza kupatikana
kutokana simu yake kuita bila mafaniko.
Tanzania Daima Jumapili, lilimtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms) ambao
hata hivyo haukujibiwa hadi gazeti hili linakwenda mtamboni.CHANZO CHA HABARI NI TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment