Kutokana na hatua ya Samson Mwigamba, aliyesimamishwa uenyekiti wa
CHADEMA Mkoa wa Arusha, kukiri mbele ya waandishi wa habari kuwa amevunja
katiba, kanuni, maadili, miongozo, taratibu na itifaki za chama kwamba yeye
ndiye aliyeandika (kwa kutumia jina bandia);
Kwenye mitandao ya kijamii, waraka uliojaa uongo, upotoshaji na
uchonganishi kwa wanachama na viongozi, Idara ya Habari ya CHADEMA (kupitia
Ofisa Habari, ambaye alikuwepo kwenye kikao hicho) imechukua hatua ya kuanza kutoa
na kuandaa utolewaji wa taarifa rasmi zinazojibu uongo, upotoshaji na
uchonganishi ulioandikwa na Mwigamba, ili kuweka kumbumbu sawa, wanachama na
Watanzania wote waelewe.
Kwa kuanzia, leo tunatoa ufafanuzi juu ya suala la kikatiba la
ukomo wa uongozi ndani ya chama.
Kupitia taarifa hii ya Idara ya Habari, kwanza tunapenda
kushangazwa na hatua ya Mwigamba kuendelea kuvunja katiba, kanuni, maadili,
miongozo, taratibu na itifaki ya chama, ambapo kupitia vyombo vya habari
ameendelea kutunga mambo yasiyokuwepo badala ya kuwasilisha hoja zake (kama
anazo) kupitia vikao halali vya chama ambavyo yeye anao uwezo wa kuitisha au
kuhudhuria.
Tungependa umma ufahamu masuala kadhaa, kwamba katika kikao cha
Baraza la Uongozi wa Kanda ya Kaskazini (Tanga, Manyara, Kilimnajaro a Arusha),
muda mfupi kabla Mwigamba hajatuhumiwa kwa usaliti na hujuma, alikuwa ametoka
kuwasilisha taarifa ya hali ya chama katika mkoa wa Arusha.
Kupitia taarifa yake hiyo Mwigamba alisifia viongozi wa chama
taifa kwa kusimamia maslahi na matakwa ya Watanzania katika hoja au agenda
mbalimbali pamoja na kuendesha chama vizuri. Akamsifia Mbunge wa Arusha Mjini,
kwa juhudi zake za uenezi na uimarishaji wa chama.
Aidha baada ya kubainika kwa tuhuma hizo, pamoja na uthibitisho
uliokuwa chini ya waraka huo, uliotumika na wataalam wa kompyuta kubainisha
pasi na shaka kuwa waraka ule umetoka na umehifadhiwa kwenye kompyuta yake, Mwigamba
alipoulizwa alikana kabisa mbele ya kikao, akisema hahusiki wala haijui
‘article’ ile ilitokea wapi, hadi alipolazimika kuandika maelezo yak echini ya
kiapo.
Jana mbele ya waandishi wa habari ameendelea ‘kugeuka-geuka’,
akizungumza lugha tofauti tofauti kwenye suala moja.
Pili, kupitia taarifa hii kwa umma, Idara ya Habari ya CHADEMA,
inaweka hapa chini kumbukumbu sahihi juu ya kauli ya upotoshaji, uongo na
uchonganishi ya Mwigamba kuwa uongozi wa juu wa chama ‘umechakachua’ katiba kwa
kuondoa kipengele cha ukomo wa kushika madaraka ya uongozi ndani ya chama.
Kumbukumbu hii sahihi inatokana na ufafanuzi uliotolewa katika
mitandao ya kijamii (baada ya kuombwa na watu wengi) na Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi, John Mnyika, ambaye alikuwa Katibu wa Kamati iliyohusika na uandikaji
upya wa Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006, ambayo ndiyo inatumika hadi sasa.
Ufafanuzi wenyewe
ni huu (una sehemu mbili, kwa nafasi yake, pia maoni yake binafsi).Madai ya kwamba “Wakati tukifanya mabadiliko ya katiba mwaka 2006
hatukugusa kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa
zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitanomitano. Lakini wakati katiba inachapwa
chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela”; hayana ukweli
kwa kadiri ya ufahamu wangu.
Mosi, mwaka 2006 hatukufanya marekebisho ya katiba
bali tuliandika upya katiba ya chama kutoka ile ya mwaka 2004. Waraka
uliandikwa nchi nzima kwa wanachama kutoa maoni na kuwasilisha makao makuu
kuanzia kwenye ngazi zao za chini za kikatiba.
Baada ya kukusanya maoni kulikuwa na timu tatu, timu
moja ilihusu kuandika falsafa na itikadi ya chama ambayo Mwenyekiti wake alikuwa
Profesa Baregu na katibu wake nilikuwa mimi.
Sehemu hiyo ya katiba niliandika neno kwa neno
mapendekezo ya awali kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa, tulifanya mapitio
pamoja na Profesa Baregu na hatimaye ikaingia kwenye vikao vya kikatiba vya chama
na kupitishwa.
Sehemu ya falsafa kwa sehemu kubwa tulinukuu kwenye
katiba kama ilivyokuwa mwaka 2004, sehemu ya itikadi tuliandika upya kabisa
haikuwepo katika katiba ya CHADEMA ya zamani.
Sehemu zingine katika katiba kwa sehemu kubwa kazi ya
kuunganisha maoni mapya na kufanya pia rejea kwenye katiba ya zamani ilifanywa
na timu ya watu watatu tukiongozwa na muasisi wa chama Mzee Victor Kimesera
pamoja na Mkurugenzi Benson Kigaila na mimi.
Kulikuwa na timu nyingine ya kuandaa miongozo ya
mabaraza ya chama: Baraza la Wazee, BAVICHA na BAWACHA ambao nao walifanya kazi
kwa upande wao na nilishiriki katika kupendekeza mwelekeo na mapitio ya
kulinganisha rasimu ya miongozo yao na rasimu ya katiba ya chama.
Kwa ninavyokumbuka hicho kinachoitwa “kipengele kinachomzuia
kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka
mitano mitano” hakijawahi kuingizwa kwenye katiba mpya ya CHADEMA.
Baada ya timu zote kufanya kazi yake; rasimu ya
katiba ilipita katika vikao vyote vya kikatiba yaani sekretariati, kamati kuu,
baraza kuu na hatimaye mkutano mkuu. Katika vikao vyote hivyo, iwapo kipengele
hicho kingekuwa kimeondolewa ‘kinyemela’ kama inavyodaiwa, mwandishi wa tuhuma
hiyo angehoji toka Agosti 2006.
Aidha, baada ya katiba kupitishwa na kuanza kutumika
kifungu hicho kingekuwa kimeondolewa kinyemela kati ya mwaka 2006 mpaka 2008
mtoa madai au mtu mwingine yeyote ndani ya chama angekuwa amehoji wakati wa
matumizi. Kumekuwepo pia mchakato wa kufanya marejeo kwa ajili ya kushughulikia
makosa ya uchapaji (errata) kwa nyakati mbalimbali, suala hili si kati ya mambo
yaliyoibuliwa.
Mwaka 2009 CHADEMA kilifanya uchaguzi mkuu wakae mkuu
nchi nzima ambapo vifungu vya masuala ya uchaguzi wa ndani ya chama vilifanyiwa
rejea mara kwa mara. Mwandishi wa madai hayo alikuwepo wakati huo, suala hili
la kwamba kuna kifungu kimeondolewa kinyemela sikulisikia likilalamikiwa kwenye
vikao vyovyote vya kikatiba iwe ni sekretariati, kamati kuu, baraza kuu na
mkutano mkuu.
Kwa vyovyote vile kwa historia ya chama toka mwaka
kilipoanzishwa mpaka wakati huo wa uchaguzi wapo viongozi ambao walikuwa
wanagombea wakiwa na vipindi viwili wakati huo kwenye cheo kimoja cha ngazi
moja; kifungu hicho kingekuwepo toka 2006 kingetumika kuwawekea mapingamizi. Na
kama kingekuwa ‘kimeondolewa kinyemela’ kungekuwa na malalamiko mengi kiko wapi
kwa kuzingatia ‘joto’ la uchaguzi wa wakati huo.
2010 mpaka 2013 madai hayo hayajawahi kutolewa kwenye
kikao chochote cha kikatiba katika ngazi ya taifa kwa kuwa mimi ni mjumbe wa
vikao vyote vya kitaifa ambavyo yeye amesema kwamba ni mjumbe.
Madai kama hayo yangetolewa na asiye mwanachama au
walau mwanachama wa kawaida tungesema tu ni maoni ya kawaida yaheshimiwe na
aelimishwe. Lakini madai kama hayo yakitolewa na kiongozi wa chama mwenye
nafasi ya kuujua ukweli wote huo yanaacha maswali kuhusu dhamira yake. Naamini
mamlaka zinazohusika za chama zitatumika katiba, kanuni, maadili na itifaki
kuchunguza na kuchukua hatua kuanzia kwenye ngazi yao huko tukio lilipotokea.
Maoni binafsi ya John Mnyika
katika suala hili
Hata hivyo, kwa maoni binafsi (yasichukuliwe kuwa ni
kauli ya nafasi ninazoshikilia kwenye chama), dhamira ya haya inajionyesha
kwenye andiko lenyewe la muhusika kuanzia aya ya kwaza “ Kufuatia malumbano
yanayoendelea kwenye vyombo vya habari namadhaifu mengi ambayo
tumeshayashuhudia kwenye chama kwa sasa, natoa wito kwawana CHADEMA wote nchini
kwamba wakati umefika tubadilishe uongozi wa juu wachama.
Mtoa madai anaendelea kuandika kwamba “ Ni muhimu
wanachadema mkafahamu kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho
kinacholeta mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania
uenyekiti. Kama kingekuwepoleo Mbowe alikuwa anakatazwa na katiba kugombea
kipindi cha tatu na hivyo vita iliyopo kati yake na Zitto isingekuwepo na chama
kingekuwa imara zaidi. Ni dhahiri Mbowe aliondoa kipengele hicho kwa makusudi
ili aweze kuendelea kugombea bila mwisho na huu ni udikteta kama ule tu wa
akina Lyatonga Mrema, John Cheyo na wengineo, na wanachadema hatupaswi
kuuruhusu si kwa Mbowe tu balikwa yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti
wa chama chetu.
Anaendelea kuandika madai mengine mengi ya upotoshaji
lakini mwishoni anamalizia kwa dhamira yake ile ile “Nitaendelea kuwadondolea
ili muonekwa nini napendekeza tuung'oe uongozi huu chini ya Mbowe.”. Kwa hiyo,
dhamira yake ni uchaguzi na mabadiliko ya uongozi; dhamira yeyote njema ifuate
mkondo wa katiba, kanuni, maadili na itifaki; kinyume chake ni ‘njama ovu’ na
‘utovu wa maadili”.
Nimekuwepo chaguzi mbili kuu za CHADEMA 2004 (nikiwa
mtazamaji sio mwanachama) na 2009 nikiwa katikati ya chaguzi hizo kama
kiongozi. Naamini uchaguzi huu wa chama ulioanza kuanzia mwaka huu 2013
utakamilika mwaka 2014 CHADEMA ikiendelea kusimamia dhima yake ya kuleta
uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa
maendeleo endelevu ya nchi yetu.
JJ
Imetolewa leo Jumanne, Oktoba 29, 2013 na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari-CHADEMA
No comments:
Post a Comment