Nani akuulize ulipo zaidi ya mwenza wako? Mwanzo wakati mnakutana, maswali haya huwa chagizo kubwa sana, kila mmoja hupenda kumuuliza mwenzake alipo, anafanya nini, atarudi saa ngapi na zawadi gani atarudi nayo.
Taratibu mambo huanza kubadilika watu wanapokuwa wamezoeana, raha zetu za wakati ule zinaanza kuwa karaha. Hivi karibuni nilikutana na rafiki yangu mmoja aliyenipa mkasa wake na mke wake. Aliniambia wamekorofishana sana kiasi kwamba hivi sasa anahisi ndoa yake inaweza kuanguka wakati wowote.
Alinipa sababu hasa za hali kufikia hapo. Kitu kikubwa kilichosababisha hali hiyo ni kitendo cha mkewe kumchunguza sana, hasa kuikagua simu yake na kufuatilia kila simu au sms zinazoingia.
Kitendo hicho kilimkera, akaamua kumpiga mke wake na sasa wana wiki ya pili hawaongei na hakuna dalili kama hali hiyo inaweza kubadilika katika siku chache zijazo. Ana hofu, huenda mwanamke akaamua kurudi kwao!
Nilimpa moyo. Kama mmegombana hadi kupigana na hii ni wiki ya pili sasa, uwezekano wa kuondoka ni mdogo. Lakini pia, nilimtaka kutambua kwamba misuguano katika maisha ya kimapenzi ni jambo la kawaida kabisa.
Usishangae kusikia watu wamekaa ndani ya nyumba yao wiki mbili bila kuzungumza, hili lipo na litaendelea kuwepo katika ulimwengu wa mapenzi.
Yanayotutokea katika nyumba au uhusiano wetu, yana nafuu kuliko ya wenzetu ambayo hatuyajui. Usione mtu na mkewe wanacheka na kuonyesha furaha kubwa mnapowatembelea majumbani mwao, huwezi jua, huenda huu ni mwaka sasa hawazungumzi.
Mwanaume anatekeleza majukumu yake ya kulea familia kama kawaida, anasomesha watoto, anaacha hela ya kula mezani, anawajali watoto. Mama naye anakuwa kama hivyo, anatimiza majukumu yake vizuri, anawaogesha watoto, anahakikisha hawakosi shule. Na wote kwa pamoja, wanakuwa kitu kimoja kwa wageni wanaofika, awe ndugu wa mama au wa baba, siyo rahisi kugundua kama kuna tofauti yo yote.
Watafanya hayo yote vizuri, lakini linapokuja suala la wao wawili, hakuna kupiga stori, kila mtu kimpango wake. Chumbani baba yuko bize na simu yake, hali kadhalika mama naye yupo bize kivyake.
Wakati nikiwashauri kuwa watulivu wakati wa hali kama hii, ni vyema pia kukumbuka kwamba migogoro inayosababisha hali hii, ni hatari, siyo tu kwa ustawi wa familia husika, bali hata nje yao.
Upendo wetu, iwe kwa watoto, majirani na ndugu huwa ni unafiki. Hatuwezi kuwapenda wapendwa wetu endapo sisi wenyewe tumenuniana. Tutashindwa kuwaelekeza watoto kwa sababu kila mmoja atapunguza umakini kwa makusudi!
CHANZO NI GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment