MAWAZIRI wanne wa wizara zenye dhamana ya mifugo, kilimo, ardhi na usalama, wametumwa wilayani Mvomero mkoani Morogoro kutafuta suluhu kwenye mgogoro kati ya wafugaji na wakulima katika Bonde la Mgongola.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, ndiye Mwenyekiti wa ujumbe huo uliotumwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwenda kutafuta suluhu.
Mbali na mawaziri husika, Mbunge wa Mvomero ambaye ni Naibu Waziri wa Habari ,Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla alihudhuria kikao cha mawaziri hao, kabla ya mawaziri hao kukutana na wananchi kusikiliza hoja zao.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika Kijiji cha Mkundo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck ole Medeye, alisema mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu na kusababisha mauaji ya mara kwa mara.
Alisema shauri kuhusu mgogoro huo ulioko mahakamani halijamalizika na kesi hiyo imekuwepo Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi bila kusikilizwa kwa miaka minane sasa.
Hata hivyo alisema hawawezi kuingilia Mahakama isipokuwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake, kusukuma suala hilo lipewe kipaumbele na limalizwe mapema.
“Tutashauri Mahakama isikilizwe, na ikimalizika pande mbili hizi zikutane ili kufikia muafaka wa kudumu,” alisema Medeye.
Aliagiza mamlaka za upimaji ardhi, zihakiki upya kujua wamiliki wa ardhi husika na baada ya hapo, eneo hilo lipimwe na watu wamilikishwe na wenye haki wafaidike nalo.
Katika mkutano huo, Chiza alisema ni muhimu matatizo ya wananchi yafanyiwe kazi kwa haraka na kutoa majibu sahihi kwa wakati badala ya kusubiri matukio ikiwemo mauaji.
“Tusifanye kazi kwa kusubiri matukio kama haya ya mauaji, tufanyie kazi masuala ya ardhi bila kusubiri kutokea maafa, nafikiri sasa tujisahihishe... siyo waziri aje hapa kuona watu wameuawa,” alisema Waziri Chiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, akizungumza kwenye mkutano huo, alieleza kutoridhishwa na utendaji kazi wa Polisi hasa katika operesheni ya kukamata ya watuhumiwa wa vurugu kutoka pande zote.
Dk Nchimbi alishangazwa kuona watuhumiwa 32 waliokamatwa wakati wa vurugu na mapingano hayo, wafugaji wakiwa wawili pekee.
Alisema katika mapigano hayo, watu sita waliouawa na kati ya hao wakulima ni wanne na wafugaji ni wawili na kuwakamata wakulima wengi tofauti na wafugaji, kunaleta maswali na shaka.
Waziri Nchimbi alimwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, kusaka watuhumiwa wengine hususan wafugaji waliohusika kwenye vurugu na mauaji hayo.
Aliagiza watuhumiwa wachujwe haraka na watakaobainika kutohusika waachiwe mara moja.
Awali, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo David, alitaka wafugaji kufuata utaratibu wa sheria na kuzingatia nchi ina wakulima, wafanyakazi na wafugaji.
Aliagiza watuhumiwa wachujwe haraka na watakaobainika kutohusika waachiwe mara moja.
Awali, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo David, alitaka wafugaji kufuata utaratibu wa sheria na kuzingatia nchi ina wakulima, wafanyakazi na wafugaji.
Alisema sababu za wafugaji kwenda maeneo ya wakulima ni ukosefu wa miundombinu maeneo ya vijijini hasa majosho na maji. Dk Mathayo alitaka halmashauri zenye maeneo ya wafugaji ziweke miumbombinu kwa ajili ya mifugo.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment