Marehemu Dunia Mzobora enzi za uhai wake.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni na
Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara kufuatia kifo cha Mwandishi
wa Habari na Msanifu wa Habari Msaidizi Mkuu wa Gazeti la Uhuru, Bwana
Dunia Mzobora, kilichotokea tarehe 27 Novemba, 2013 katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amepelekwa kwa matibabu ya shinikizo
la damu.
Marehemu
aliajiriwa katika Magazeti ya Uhuru na Mzalendo mwaka 1989 kama
Mwandishi wa Habari Mwanafunzi, kisha akaendelea kupanda ngazi hadi
kufikia cheo cha Msanifu wa Habari na hatimaye kuwa Msanifu Mkuu
Msaidizi, cheo alichokuwa akikishikilia hadi mauti yalipomkuta.
“Nimesikitishwa
na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha mmoja wa Waandishi wa Habari
Shupavu na Mchapakazi, Dunia Mzobora aliyekuwa akilitumikia Gazeti la
Chama Cha Mapinduzi (CCM) la UHURU, kilichosababishwa na ugonjwa wa
shinikizo la damu baada ya kuwa amepelekwa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili kupatiwa matibabu”, amesema kwa masikitiko Rais Kikwete.
Rais
Kikwete amesema binafsi alimfahamu vyema Marehemu Dunia Mzobora, enzi za
uhai wake, kama Mwandishi wa Habari aliyejituma vilivyo katika kazi
zake za kuuhabarisha, kuuelimisha na kuuburudisha Umma kwa kutumia vyema
kalamu yake, na kwa kuzingatia kikamilifu Maadili ya Taaluma yake ya
Uandishi wa Habari.
“Kufuatia
taarifa za kifo cha Dunia Mzobora, ninakutumia wewe Waziri wa Habari,
Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara na Wafanyakazi
wote wa Kampuni ya Magazeti ya Chama ya Uhuru na Mzalendo na kwa kweli
Waandishi wote wa Habari nchini, Salamu zangu za Rambirambi kwa
kumpoteza mmoja wa Waandishi wa Habari Mahiri ambaye amelitumikia vyema
Taifa lake kupitia Tasnia ya Habari”.
“Aidha
kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi na pole
nyingi kwa Familia ya Marehemu Dunia Mzobora kwa kumpoteza Baba,
Kiongozi na Mhimili wa Familia”.
Rais
Kikwete amewahakikishia Wanafamilia kuwa yeye binafsi yuko pamoja nao
katika kuomboleza msiba wa mpendwa wao, na anamuomba Mwenyezi Mungu,
Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu
Dunia Mzobora, Amina.
Rais
Kikwete amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira katika
kipindi hiki kigumu wanachopitia baada ya kumpoteza mtu muhimu aliyekuwa
kiungo cha Familia yao, kwani yote ni Mapenzi yake Mola.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment