MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi
(61), amefariki, katika hospitali ya Milpark, nchini Afrika Kusini
alikopelekwa kwa ajili ya matibabu zaidi.
Marehemu Dk. Sengondo Mvungi enzi za uhai wake.
Dk. Mvungi, mwanasheria maarufu nchini na mwanachama wa NCCR-Mageuzi,
alivamiwa Novemba 3, mwaka huu saa 6:30 usiku na watu wanaosadikiwa
kuwa majambazi, nyumbani kwake Kibamba, Kata ya Mpiji Magohe, nje
kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kujeruhiwa kwa mapanga sehemu za
kichwani na usoni.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi,
James Mbatia, alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa hizo na
kuwa chama hicho kimepoteza kiongozi makini, na pengo lake haliwezi
kuzibika.
“Ni kweli tumepata taarifa hizo, mwenzetu hatunaye tena, ni huzuni
kwa chama na Watanzania tutamkumbuka kwa mambo mengi ndani ya chama,
hata taifa,” alisema.
Alisema kuwa Dk. Mvungi alifariki dunia jana saa 9:30 katika
hospitali hiyo ambako alihamishiwa Novemba 8, mwaka huu akitokea katika
Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI).
Naye Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Freeman Mbowe, alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo
Dk. Mvungi.
Mbowe alisema kuwa CHADEMA kinatoa pole kwa familia, chama cha
NCCR-Mageuzi, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na
Watanzania wote kwa kupoteza mtu makini na muhimu katika mustakabali wa
taifa letu.
“Nimepokea taarifa hizo kwa masikitiko kwa kuwa Dk. Mvungi ni
mmojawapo wa waasisi wa mageuzi nchini, ambaye hakukata tamaa kutumia
taaluma yake. Mungu ana mipango yake, huyu ndugu alijitahidi kupigania
suala la katiba mpya kwa miaka 20, na akateuliwa aiandae, tunasikitika
kwa kuwa hataona katiba mpya yenye mawazo yake,” alisema.
Alisema kuwa tume inapaswa kuendeleza mawazo na michango aliyokuwa akisaidia katika kuandaliwa kwa katiba mpya.
Aidha, taarifa ya kifo cha mwanasheria huyo ilisambaa kwa kasi katika
mitandao mbalimbali ya kijamii, huku wadau wa mitandao hiyo
wakionekana kushitushwa na kuwataka Watanzania kuwa na subira kwa
wakati huu mgumu.
Baadhi yao walienda mbali zaidi na kuhoji juu ya mchakato wa kupata
katiba mpya utakapoishia kutokana na kuwa mwanasheria huyo ni mtu
muhimu kwenye majukumu ya tume, kwani amebobea katika masuala ya
katiba.
Aidha, kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein Bashe, katika
ukurasa wake aliandika kuwa wahalifu wamekatisha uhai wa kiongozi huyo
wakati akitekeleza jukumu zito kwa ajili ya maslai ya taifa letu.
“Dk. Sengondo Mvungi is no more, taarifa zilizonifikia kutoka
Millpark hospitali ndugu yetu Dk. Mvungi amefariki saa 9:30. Mungu
ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi,” alisema Bashe.
Alisema kuwa jambo hilo linaumiza sana na Mungu atalipia uhalifu huo,
na kuitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba na NCCR-Mageuzi kuwa
wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Dk. Mvungi alivamiwa nyumbani kwake na watu wasiojulikana ambao kwa
mujibu wa Mbatia, kabla ya kuvunja milango ya nyumba, walilipua kitu
ambacho kilitoa moshi mwingi na cheche kisha kuingia ndani na kuanza
kudai wapewe fedha.
Mbatia alisema kuwa hatua hiyo ilisababisha Dk. Mvungi kupambana nao
bila mafanikio, ndipo wakamjeruhi vibaya kwa kumcharanga mapanga
kichwani, usoni na kisha kuondoka na kompyuta mpakato (Laptop) yake,
pisto na kiasi cha fedha ambacho hakijajulikana.
Mbatia alisema majirani na ndugu walifanikiwa kumbeba Dk. Mvungi na
kumkimbiza katika hospitali ya Tumbi mkoani Pwani ambako alipatiwa
matibabu ya awali na kisha kuhamishiwa Muhimbili saa 10:00 alfajiri.
Dk Mvungi ambaye alikuwa hajitambui alitolewa na kuingizwa kwenye
gari la wagonjwa lenye namba za usajili STK 8767, akipelekwa katika
Hospitali ya Aghakan kwa ajili ya kufanyiwa kipimo cha CT-SCAN kwa
ajili ya kuona ameathiriwa vipi katika eneo la kichwa.
Alilazimika kupelekwa kupimwa kipimo hicho Aghakan na kisha arejeshwe
kwa sababu uongozi wa MOI uliwaeleza kuwa mtaalamu anayefahamu kutumia
kipimo hicho hakuweza kupatikana mara moja.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment