TAARIFA KWA UMMA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumamosi, Januari 18, 2014,
amefanya uteuzi wa Makatibu Tawala wapya wa mikoa mitano na kuhamisha
makatibu tawala wengine na Wakurugenzi wa Majiji nchini.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi (KMK),
Balozi Ombeni Sefue iliyotolewa jioni ya leo, Ikulu, Dar Es Salaam
inasema kuwa uteuzi na uhamisho huo unaanza leo hii.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makatibu
Tawala wapya ni Ndugu Wamoja A. Dickolangwa ambaye ameteuliwa kuwa
Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa ambako alikuwa Kaimu Katibu Tawala;
Ndugu Abdallah D. Chikota ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa
wa Lindi. Kabla ya hapo, alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri wa Wilaya ya
Newala na Ndugu Symthies E. Pangisa ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala
wa Mkoa wa Rukwa. Kabla ya uteuzi wake, Ndugu Pangisa alikuwa Kaimu
Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara.
Wengine ni Ndugu Alfred C. Luanda ambaye
ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara. Kabla ya uteuzi wake,
alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na Ndugu Jackson
L. Saitabau ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.
Kabla ya hapo, alikuwa Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Arusha.
Taarifa hiyo iliwataja waliohamishwa kuwa
ni Ndugu Beatha Swai aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani na sasa
anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI; Ndugu Sipora J. Liana
ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha anahamishiwa Ofisi ya Waziri
Mkuu, TAMISEMI; Ndugu Benedict Ole Kuyan ambaye alikuwa Katibu Tawala
wa Mkoa wa Tanga anahamishiwa Mkoa wa Mara na Ndugu Salum M.Chima ambaye
alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa anahamishiwa Mkoa wa Tanga.
Wengine waliohamishwa ni Ndugu Mgeni
Baruani ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe anahamishiwa Mkoa
wa Pwani; Ndugu Juma R. Iddi ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya
anahamishiwa Jiji la Arusha kama Mkurugenzi; Eng. Omari Chambo ambaye
alikuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi anahamishiwa Mkoa wa Manyara
kama Katibu Tawala wa Mkoa huo na Dkt. John Ndunguru aliyekuwa Naibu
Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi anahamishiwa Mkoa wa Kigoma kama Katibu
Tawala wa Mkoa huo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
18 Januari, 2014
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
18 Januari, 2014
No comments:
Post a Comment