KAMA ilivyo kawaida ya kila siku, ni budi kumshukuru Mwenyezi Mungu
kwa kutubariki tena leo, tukikutana tukiwa na uwezo wa kutambua kwamba,
bila yeye aliye juu, tusingeweza kuwa pamoja.
Wema wa Mungu umetufanya tuendelee kushikamana kama taifa na tunaishi
kama moja ya mifano bora kabisa ya amani katika ukanda huu wa Afrika
Mashariki. Hii ni tunu ambayo yatupasa kuitunza na moja ya njia za
kutufanya tuifanikishe, ni kuishi katika kumuamini Mungu na kujiweka
tayari kwa kumtumikia.
Baada ya kusema hayo sasa tugeukie kwenye hoja yetu ya leo. Hatimaye
Rais Jakaya Kikwete ametangaza majina ya wajumbe 201 ambao wataungana na
wabunge wa sasa katika kikao cha Bunge maalum la Katiba, watakaokuwa na
kazi moja tu ya kujadili katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kama ilivyopendekezwa katika rasimu iliyokuwa chini ya
Uenyekiti wa Jaji Joseph Sinde Warioba.
Haikuwa kazi rahisi kwa Rais kuifanya kazi hiyo, kwani kabla ya hapo,
taasisi zipatazo 554 za Tanzania Bara ziliwasilisha majina ya wajumbe
2762 na 178 kutoka Zanzibar zilizokuwa na majina 874. Ni katika majina
hayo, ndipo Rais Kikwete na mwenzake wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein
waliweza kuyajadili na hatimaye kufikia kuwatangaza waliotangazwa.
Ni hatua ya kupongezwa sana kwani kwa vyovyote vile, ilikuwa ni kazi
ngumu iliyohitaji umakini mkubwa, hasa kwa jambo kubwa na muhimu
linalokwenda kufanywa na wateule hao. Aidha, majukumu mengi na mazito ya
kikazi ya viongozi hao wawili, yalichangia kuifanya kazi hiyo kuwa
ngumu zaidi.
Hii ni hatua moja muhimu sana katika mustakabali wa nchi yetu,
wanachokwenda kukifanya wateule hao ni kuamua kuhusu uhai wa taifa letu.
Kuna jambo moja tu ambalo Watanzania wote tunaweza kulisema juu ya
watu wote watakaoingia ndani ya Bunge hili, nalo ni kututendea haki sisi
pamoja na taifa letu kwa ujumla.
Ninafahamu kwamba watu watakaokwenda huko, wako na masilahi kutokana
na makundi wanayowakilisha, kama walemavu, wanasiasa, kutoka asasi
zisizo za kiserikali na kadhalika.
Ninajua, kila mtu atataka
kuwakilisha kundi lake, kwa vile kama tunavyojua, majina yao yalitumwa
na taasisi zao wakiamini kabisa wakiteuliwa, watatanguliza masilahi ya
asasi zao.
Lazima niseme kwamba pamoja na umuhimu wa kuwasilisha maoni ya
taasisi wanazotoka, lakini jambo la msingi kabisa ni kila mmoja wao
kuzingatia kwamba tunachotaka kukiona mwisho wa siku zao bungeni, ni
katiba ambayo itakuwa imetoa upendeleo mkubwa mno kwa mtu mmoja
anayeitwa Mtanzania.
Mtu huyu, wote tunajua kuwa siyo mwanasiasa, siyo mlemavu, siyo mkulima, mfanyabiashara wala mwingine.
Ni mtu anayesimama katikati ya vitu vyote hivi, lakini kwa bahati
mbaya sana, hataweza kuingia ndani ya jumbe lile pale Dodoma kutokana na
ukubwa wake. Anahitaji watu walioteuliwa wiki iliyopita, wazungumze kwa
niaba yake.
Kama wateule hawa wataingia ndani ya jumbe lile na kuanza kuzungumza
kuhusu masilahi ya asasi iliyompeleka huku akimtelekeza Mtanzania,
hakika itakuwa ni usaliti mkubwa sana. Tunawasihi wampiganie, kwa sababu
huyu akinyimwa haki yake, hakutakuwa na maana na bunge hilo litapoteza
uhalali wake.
Tunataka kila mjumbe, aisikilize hoja, aipime, kwanza kwa kuangalia
umuhimu wake kwa wananchi, halafu atoe maoni yake yenye kuboresha au
kupinga. Hatutaki hoja kuungwa mkono kwa sababu tu, kundi lililowatuma
linataka hivyo.
Ni lazima tutambue kwamba Watanzania ni muhimu zaidi kuliko wafuasi
wote wa vyama, ni zaidi ya madhehebu yote ya kidini, ni zaidi ya asasi
zote zisizo za kiserikali na kusema kweli, Tanzania ni zaidi ya kila
kitu.
Kwa maana hiyo, mjadala huo usigeuzwe sehemu ya kushambuliana kwa
misingi ya vyama au makundi, tunataka tuwaone wajumbe hawa wakiiweka
mbele Tanzania na watu wake, kwa sababu hiyo ndiyo hasa sababu ya
kuanzishwa na hatimaye kutekelezwa kwa mabadiliko ya katiba, ambayo
tunataka ikidhi mahitaji yetu ya sasa kama taifa.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
No comments:
Post a Comment