Stori: Mwandishi wetu, Dodoma
Pongezi! Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda juzi Jumamosi alikabidhi Tuzo ya Mwanamke Bora wa Mwaka (A Woman of the Year Award- 2013/14) mjini hapa.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda (kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni tano Dk. Maria Kamm aliyetwaa Tuzo ya Mwanamke Bora wa Mwaka 2013/2014 ndani ya Ukumbi wa African Dreams uliopo Area D, Dodoma.
Katika kinyang’anyiro hicho, Dk. Maria Kamm, ambaye kitaaluma ni mwalimu, aliibuka kidedea na kunyakua tuzo hiyo, medali pamoja na hundi ya shilingi milioni 5.
Wengine walionyakua tuzo hizo (bila medali) ni pamoja na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha Rose Migiro (aliwakilishwa na Anna Abdalah), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Mbunge wa Same Mashariki, Mheshimiwa Anne Kilango Malecela.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda (kushoto) akimvisha medali ya Mwanamke Bora wa Mwaka 2013/2014, Dk. Maria Kamm.
Katika tukio hilo la kufana lililofanyika katika ukumbi wa kisasa wa The African Dream nyakati za usiku, watu mbalimbali maarufu walihudhuria wakiwemo wajumbe wengi wa Bunge Maalum la Katiba wanaoendelea na vikao vyao mjini hapa.
Waziri Mkuu akimkabidhi tuzo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Profesa Anna Tibaijuka aliyeibuka mshindi wa tatu katika tuzo hizo.
Tuzo hizo zilizoratibiwa na Global Publishers Ltd zilianzishwa Juni mwaka jana, kwa lengo la kuheshimu, kuenzi na kuthamini mchango wa mwanamke katika jamii ya Kitanzania na zitakuwa zikitolewa kila mwaka.Jumla ya wanawake 150 walipigiwa kura ambapo baada ya miezi miwili, wanawake 20 waliongoza orodha hiyo na kuingia awamu ya pili. Baada ya muda kama huo, akina mama watano wakaingia katika awamu ya mwisho ambayo iliwatoa washindi hao.
LIVE KUTOKA TUZO YA MWANAMKE BORA DODOMA
wiki hii Live Dijitali imekuja kivingine. Baadhi ya maripota wake walipigwa kadi nyekundu hivyo wiki hii watakuwa nje ya uwanja.
Mkuu aliyekuwa Makao Makuu Bamaga-Mwenge aliwasiliana moja kwa moja na Richard Bukos ‘Mpigapicha Mkuu’ ambaye aliripoti laivu kutoka kwenye Ukumbi wa The African Dream mjini Dodoma. Alikuwa akiripoti matukio mbalimbali yaliyojiri kwenye Tuzo za Mwanamke Bora wa Mwaka (A Woman of the Year Award) 2013/14 zilizoandaliwa kwa mara ya kwanza na Kampuni ya Global Publishers.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda (katikati) katika picha ya pamoja na washindi walioingia Nne Bora. Kutoka kushoto; Anna Abdallah aliyechukuwa tuzo kwa niaba ya Dk. Asha-Rose Migiro, Anne Kilango Malecela, Dk. Maria Kamm na Profesa Anna Tibaijuka.
SAA 2:45 USIKU
KUWASILI UKUMBINI
Makao Makuu: Bukos leo mzigo utaupiga mwenyewe kwa sababu tunataka ‘pakeji’ ya kutosha kutoka kwenye tuzo hizo. Sema nini kinaendelea hapo ukumbini kwa sasa?
Bukos: Mkuu hapa ndiyo wageni waalikwa wanajiweka sawa, tayari nimemuona mama Kamm kaingia na hapa pia namuona mheshimiwa Magreth Sitta anasalimiana na mama Kamm.
Makao Makuu: Sawa, basi wewe utakuwa unanijuza kila linalotokea.
Waziri Mkuu akiwa katika picha ya pamoja na washindi, waandaaji wa tuzo hizo kutoka Global Publishers Ltd.
SAA 4:05 USIKU
SHIGONGO AKARIBISHA WAGENI NA MHE. PINDA
Makao Makuu: Naona unapiga vipi kuna taarifa mpya?
Bukos: Mkuu tayari mgeni rasmi ambaye ni Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda ameshafika. Hapa namuona Mkurugenzi wa Global Publishers, Eric Shigongo anakaribisha waheshimiwa waalikwa.
Makao Makuu: Baada ya kuwakaribisha waalikwa nini kinafuata?
Bukos: Mkuu sasa Shigongo anaeleza sababu zilizomfanya aandae tuzo hizo kwa kuelezea anavyofahamu umuhimu wa akina mama kisha anafafanua namna mchakato wa kuwapata washindi ulivyokuwa na mwisho anamkaribisha Mhe. Pinda.
Mkuu Mhe. Pinda anamsifia Shigongo na Kampuni ya Global Publishers kwa jumla kwa uamuzi wake wa kuandaa tuzo hizo. Pia anawasifia wote walioingia fainali na kuwaelezea anavyowajua. Anazidi kuwamwagia sifa tu na kuwapa pongezi.
SAA 4:50 USIKU
DOCUMENTARY NA TUZO
Makao Makuu: Umepita ukimya fulani Bukos, hebu nijuze sasa nini kinaendelea?
Bukos: Mhe. Pinda alipomaliza hotuba yake yenye msisimko wa aina yake ulifika muda wa kusikiliza documentary ya Profesa Tibaijuka kisha akapewa tuzo.
SAA 11:30 USIKU
NI ZAMU YA WASHINDI WENGINE
Makao Makuu: Nini kimefuata?
Bukos: Hapa kila mshindi inawekwa documentary yake kisha anakabidhiwa tuzo yake lakini cha kusisimua Mkuu ni kwa mama Kamm ambaye mbali na zawadi ametunukiwa medali na mshiko wa shilingi milioni 5.
SAA 6:04 USIKU
MAMA KAMM KIVIPI?
Makao Makuu: Bukos Kivipi?
Bukos: Mkuu lilipotajwa tu jina lake ukumbi ulisisimka asikwambie mtu huyu mama alistahili.
Makao Makuu: Kwa hiyo shughuli imekwisha?
Bukos: Hapana mkuu bado shamrashamra zinaendelea.
Makao Makuu: Wewe endelea kuchukua matukio yatapamba kwenye Gazeti la Uwazi kesho.
Bukos: Asante Mkuu, kwa uhondo mwingine wa shughuli hii ni kesho kwenye Uwazi Mkuu.
No comments:
Post a Comment