Mshambuliaji mpya wa Yanga aliyekuwa akikipiga katika timu ya Coventry City ya England Suleiman Abdallah Mbarouk.
Mshambuliaji huyo raia wa Tanzania ambaye amekuwa akicheza soka
England kwa miaka mingi, Suleiman Abdallah Mbarouk, aliyekuwa akikipiga
katika timu ya Coventry City ya England inayoshiriki Ligi Daraja la
Kwanza, alijumuika mazoezini kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola
jijini lakini bado hajapewa mkataba wowote.Taarifa kutoka klabuni hapo zinaeleza kuwa, Maximo amekabidhiwa mchezaji huyo kwa ajili ya kumfanyia majaribio na kama akionekana anaweza, atapewa mkataba.
Championi Ijumaa, lilizungumza na mchezaji huyo ambapo alisema amerejea nchini kwa kuwa mkataba wake na klabu yake nchini England ulimalizika na hakuwa kwenye mipango ya timu yoyote.
“Nimeachana na Coventry City mwaka mmoja hivi uliopita, niliumia mgongo, hivyo nikawa nje ya uwanja kwa muda wa miezi sita, lakini hivi sasa nimepona, nahitaji kuendeleza kipaji changu cha soka.
“Wakala wangu, anaitwa Salim ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Afri-Soccer cha Zanzibar, ndiye amenileta hapa kwa ajili ya majaribio, nilianzia Simba na sasa nimekuja kujaribu Yanga.”
Mchezaji huyo ambaye alisema kabla ya kutua Coventry City aliwahi kupata mafunzo ya soka katika kituo cha Chelsea cha England, hakuonyesha uwezo mkubwa katika mazoezi ya jana, hata Maximo pia hakutaka kuzungumza chochote juu yake.
Gazeti hili lilipotafuta takwimu na rekodi zake lilibaini kuwa aliwahi kuichezea timu ya watoto ya Coventry City, lakini kama anahitaji kupata nafasi kweli kwenye kikosi cha Yanga, basi kazi kubwa ipo mbele yake.
No comments:
Post a Comment