WAKATI Watanzania wakilisubiri kwa hamu Tamasha la Matumaini litakalofanyika Agosti 8, mwaka huu ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar, habari njema ni kwamba, staa wa Chuna Buzi, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ ameahidi kumkalisha mkali wa Johhny, Yemi Alade atakayekuja kulipamba tamasha hilo.
Mkali wa kudansi kutoka Nigeria, Yemi Alade akipozi.
Akizungumzia tamasha hilo lenye lengo la kuchangisha fedha kwa ajili
ya kusaidia mfuko wa elimu nchini, mratibu Luqman Maloto, amesema uwepo
wa Shilole siku hiyo utaamsha hisia za mashabiki wengi uwanjani hapo
kutokana na staili ya uimbaji na uchezaji kufanana na ya Yemi Alade.“Kawaida ya Shilole jukwaani huwa habahatishi na niwaambie tu utakuwa mchuano mkubwa siku hiyo kwani hapa Shilole pale Yemi Alade, sijui nani ataibuka kidedea wa shoo siku hiyo, mashabiki wenyewe ndiyo watakaoamua,” alisema Maloto.
Utamu wa tamasha hilo hautaishia hapo, Maloto alisema watakuwepo pia waimbaji wanaotamba kunako muziki wa Injili ambao watatoa burudani nzuri ya kumsifu Mungu.
“Listi ni ndefu na inazidi kuongezeka kila kukicha na mpaka sasa wasanii wakubwa wa muziki wa Injili tutakaokuwa nao ni pamoja na Upendo Nkone, Ambwene Mwasongwe, Angela, Paul Clement na Martha Mwaipaja,” alisema Maloto.
Maloto alisema, katika eneo la Bongo Fleva, watakuwepo wasanii lukuki kulipamba tamasha hilo kwa kiingilio cha shilingi elfu tano tu.“Bado wasanii wanaendelea kuongezeka lakini hadi sasa tumeshawaweka mkononi Madee, R.O.M.A Mkatoliki, Meninah, Juma Nature na kundi zima la Wanaume Halisi, Ali Kiba na kwa mara ya kwanza Wema Sepetu atapanda jukwaani na kuimba nyimbo za bebi wake Diamond,” alisema Maloto.
Staa wa Chuna Buzi, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ akipozi.
Aidha, tamasha hilo litajumuisha michezo mbalimbali kama vile mpira
wa miguu na ndondi ambapo mwaka huu Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu
Nchemba atazichapa na Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala.“Tutakuwa na mwanamuziki Khalid Chokoraa ambaye atazichapa ulingoni na Said Memba huku Bingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Thomas Mashali akizitwanga na ‘mbunge mtarajiwa’, Mada Maugo.
“Ushindani mkali pia utawekwa na mastaa wa Bongo Movie, Cloud 112 na Jacob Steven ‘JB’ ambao siku hiyo watazipiga katika pambano la raundi 4,” alisema Maloto.
Maloto alimaliza kwa kusema kuwa kutakuwa na mechi kali kati ya Wabunge Mashabiki wa Yanga dhidi ya wenzao wa Simba huku timu ya Bongo Movie ikiingia uwanjani kumenyana na Bongo Movie.
Tamasha hilo limedhaminiwa na kampuni ya Vodacom, Pepsi, Azam TV, EFM (93.7), Clouds FM (88.5), Sycorp pamoja na Times FM (100.5).
No comments:
Post a Comment