AGOSTI 8, mwaka huu Uwanja wa Taifa patakuwa hapatoshi kwani Watanzania watashuhudia matukio makubwa ya burudani kupitia Tamasha la Usiku wa Matumaini.
Miongoni mwa matukio hayo ni ndondi za waheshimiwa wabunge ambapo mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangala atakazichapa ‘kavukavu’ na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba.
Akizungumza na Mikito Nusunusu, Mratibu wa tamasha hilo lenye lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya sekondari nchini, Luqman Maloto alitaja burudani kibao zitakazolipamba tamasha hilo ikiwemo mechi ya wabunge mashabiki wa Simba na wenzao wa Yanga, Bongo Fleva dhidi ya Bongo Movie.
Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamis Kigwangala akiongea na wanahabari wa Global Publishers (hawapo pichani).
“Wabunge wa Yanga sasa hivi wanatamba na usajili mpya wa Ridhiwani
Kikwete wakati wenzao wa Simba wakiwa na Geodfrey Mgimwa sasa sijui
mwaka huu nani ataibuka bingwa kwani mwaka jana Yanga walishinda kwa
ushindi mdogo wa 1-0,” alisema Maloto.Yemi alade wa Nigeria kulitikisa jukwaa
Maloto alisema kwa upande wa burudani ya muziki, atadondoka mkali kutoka Nigeria anayetamba na wimbo wa Johnny, Yemi Alade ambaye ameahidi kumtafuta Johnny wake katikati ya maelfu ya mashabiki watakaojitokeza uwanjani siku hiyo.
Hapatoshi kwenye soka
Kama hiyo haitoshi, Maloto alisema katika upande wa mpira wa miguu, mwaka jana kwenye tamasha hilo mechi kati ya Bongo Movie na Bongo Fleva, Bongo Fleva waliibuka kwa ushindi wa bao 1-0 safari hii mambo yatakuwaje?
“Tayari Bongo Movie wameshataja kikosi kamili kitakachoongozwa na kipa wao mahiri Mzee Majuto ‘King’ huku wakiwa kambini chini ya kamati ya ufundi inayoongozwa na Fatuma Makongoro ‘Bi Mwenda’ wakiahidi kuwateketeza kabisa Bongo Fleva,” alisema Maloto.
Kwenye kipengele cha ndondi, Maloto alisema pia kutakuwa na kipute kikali kati ya bondia anayeshikilia mkanda wa UBO (Universal Boxing Organization), Thomas Mashali ‘Simba Asiyefugika’ atakayezipiga na mpinzani wake wa siku nyingi, Mada Maugo ‘Mbunge Mtarajiwa’ huku mwanamuziki Khalid Chokoraa akipimana ubavu na Said Memba, Jacob Steven ‘JB’ atamaliza ubishi unaoendelea kwa sasa kwa kuchapana na Cloud 112 pambano hilo likiwa na raundi nne tu.
Maloto alisema, burudani haitaishia hapo, anga la muziki litashambuliwa na Ally Saleh ‘Ali Kiba’ ambapo atapanda jukwaani na kupiga nyimbo zake zote kali sambamba na kutoa sapraizi ya ukimya wake kwa mara ya kwanza.
Mastaa wengine watakaopokezana kipaza sauti ni pamoja na Meninah, R.O.M.A Mkatoliki, Madee, Juma Nature na kundi zima la Wanaume Halisi, Wema Sepetu ambaye ataimba nyimbo za bebi wake ‘Diamond’ pamoja na wengine kibao.
“Listi ya waburudishaji ni ndefu, wasomaji waendelee kufuatilia magazeti ya Global Publishers watajuzwa kadri siku zinavyosogea,” alisema Maloto.
No comments:
Post a Comment